KENYA: WALIMU WAPINGA MPANGO WA KUTUMIA LUGHA MAMA SHULENI
Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Wilson Sossion . Picha/MAKTABA
WALIMU wamepinga vikali agizo jipya la Wizara ya Elimu linalowahitaji
kufundisha wanafunzi wa madarasa ya chini kwa lugha ya mama.
Walisema sera hiyo mpya ni ngumu kutekeleza mbali na kwamba huko ni kupiga hatua kurudi nyuma.
Kupitia vyama vyao, walimu pia walisema hawajafahamishwa kuhusu sera hiyo na hawakushauriwa wakati ilipoundwa.
Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kilitaka wizara isimamishe utekelezaji wa sera hiyo na ijadiliane na walimu kwanza.
Kwa
upande mwingine, chama cha Kuppet pia kilisema sera hiyo mpya haiwezi
kutekelezwa katika enzi hii ikizingatiwa hasa hatua za kiteknolojia
zilizopigwa na shinikizo la kuwepo kwa utangamano kati ya makabila
tofauti.
Katibu Mkuu wa Knut Wilson Sossion alisema chama hicho hakikushauriwa kwa hivyo hakiwezi kukubali sera hiyo.
“Huwezi
kutangaza sera kabla kushauriana na washikadau wakuu kwanza. Tunaomba
wizara isitishe sera hiyo ili kuwe na mashauriano, bila hilo itakuwa
vigumu kuitekeleza. Hili ni suala linalohitaji washikadau wote
waelewane,” alisema.
Mwenyekiti wa Kuppet Omboko Milemba alitaja sera hiyo kama hatua ya kurudi nyuma na isiyoweza kutekelezwa kirahisi.
“Ni sera
ya kuturudisha nyuma. Tunaomba wizara iachane nayo. Tunadhani iliundwa
na wanaume na wanawake wakongwe katika wizara ambao wana nia ya
kushinikiza kuwepo kwa sheria ambazo hazioani na jinsi mambo yalivyo kwa
sasa,” alisema.
Kulingana
na sera hiyo, walimu wa shule za msingi za umma watahitajika kufunza
wanafunzi wa darasa la nne kurudi nyuma kwa lugha ya asili. Chama hicho
kilisema wizara ilishindwa kujadiliana na washikadau wa elimu ilipounda
sera hiyo.
Kufundisha
“Wizara
inafaa ishauriane kwa upana na kila mmoja anayehusika na masuala ya
elimu. Hatukushauriwa kuhusu suala hili. Tunashangaa kuwa sera kama hii
inaweza kuanzishwa na walimu wote watahitajika kuifuata ilhali vyama
havikushauriwa,” alisema Bw Milemba kwenye mahojiano ya simu.
Katibu Mkuu wa Knut alisema kuwa lugha za mama zinaweza kutumiwa shuleni lakini zisitumiwe kama lugha ya kufundishia.
“Ikiwa
unataka kueneza lugha za mama basi zinafaa kufunzwa kama masomo lakini
lugha mbili za kitaifa zibaki kama lugha za kufundisha,” alisema Bw
Sossion.
Kwa
mujibu wa sera hiyo iliyotangazwa Jumattau, “Lugha inayotumiwa zaidi
katika eneo (lugha ya mama) itatumiwa kwa shule za chekechea na katika
madarasa ya chini (kwa watoto wenye umri wa miaka 0-8).”
Vyama
hivyo vilisema itakuwa vigumu kutekeleza agizo hilo kwa kuwa walimu
wengi hawakufunzwa jinsi ya kufundisha kwa kutumia lugha za mama.
No comments