Header Ads

Mashehe waliotekwa DRC warejea Dar

MASHEHE sita waliokuwa wametekwa na waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) wamerejea nchini jana, huku wakieleza kuwa kulitaja jina la Tanzania kumewaokoa na kifo kutoka kwa waasi hao.

Kitendo cha mashehe hao kutaja wanatokea Tanzania kimewasaidia kwani kwa mujibu wao, waasi hao walisema hawana shida na Tanzania, lakini Wakongo waliwadanganya hivyo hawawapendi.

Akizungumza baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kiongozi wa mashehe hao, Mohammed Abdallah Khamis alisema, wakiwa njiani kuelekea nchini humo walivamiwa na watu hao wakiwa na silaha za kivita kisha kutekwa na kupelekwa porini.


“Mwanzo hatukuelewa kama ni wanajeshi wa serikali au wanajeshi wa porini, tulipofika nao porini ndiyo wakajitambulisha wao ni askari wa porini na wanahitaji fedha ili watuachie ama watatuua,” alisema Khamis.

Akisimulia jinsi walivyoishi porini alisema, walikuwa wanapata tabu kwani hata chakula walikuwa wakipewa ndizi, maharage na magimbi ambayo waliambiwa wale ili wasife, huku wakati mwingine wakiteswa na waasi hao kwa kupigwa na magongo na vibao.

Alisema waasi hao walihitaji wapewe kiasi cha dola za Marekani 20,000 (zaidi ya Sh milioni 60) ili waweze kuachiwa. Khamis aliishukuru serikali ya Tanzania kwa jitihada ilizofanya ili kuhakikisha wapatikana wakiwa salama.

 “Kwa kweli tunaipongeza sana serikali ya Tanzania na DRC maana wamefanya juhudi kubwa sana za kutuokoa.

"Bora kuishi mwaka mmoja gerezani lakini si kukaa na watu wale siku moja,” alisema.

Khamis alisema, hata hivyo baadaye waliachiwa na waasi hao baada ya kuona hawana fedha lakini pia ni wazee, hivyo waliwaachia kwa huruma na hasa kwa kuzingatia hawana shida na Watanzania.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim akizungumza baada ya kuwapokea mashehe hao alisema, wakati wote serikali ilikuwa ikifuatilia suala hilo ili kujua usalama wao.

Hata hivyo, alisema kuna umuhimu kwa Watanzania wanaosafiri kwenda katika nchi tofauti kwa shughuli mbalimbali kuhakikisha wanatoa taarifa katika Balozi zilizopo katika nchi hizo ili serikali iwe na taarifa ya Watanzania hao.

“Tunaishukuru sana serikali ya Congo na jamii nzima ya watu wa Goma ambao walitoa msaada mkubwa na hata walinzi wa amani wa Congo walishiriki vizuri katika kuhakikisha mnapatikana mkiwa salama,” alisema.

Alisema kutokana na kuwa vikosi vya usalama vilikuwa vikifuatilia tukio hilo kwa ukaribu, hata baada ya kuachiwa kwa mashehe hao, vikosi hivyo vilifanikiwa kuwakamata watekaji hao.

Balozi wa Tanzania nchini DRC, Anthony Cheche alisema, baada ya kupokea taarifa hizo walifuatilia na baada ya kubaini ni Watanzania ndiyo juhudi za kuwakomboa zikaanza.

Alisema alikuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa vyombo vya habari na ndugu, jamaa na marafiki za kutaka kujua hali za mashehe hao lakini wakati mwingine alilazimika kuficha ukweli ili kuepusha kuhatarisha usalama wa mashehe hao.

“Tulipewa tahadhari kuwa kuna mazingira hatarishi, hivyo kuna baadhi ya taarifa zikitolewa zinaweza kusababisha tukawapoteza watu wetu na ndiyo sababu kuna taarifa nilikuwa nikiziminya,” alisema.

Baada ya kuachiwa kwa mashehe hao ambao wote ni wakazi wa Zanzibar, walipokewa na Jeshi la DRC na kupewa ulinzi hadi Mji wa Goma ambapo walikutana na viongozi wa mji huo pamoja na Balozi Cheche ambaye waliondoka naye hadi mjini Kigali, Rwanda kwa ajili ya kurejea nchini.

Mashehe hao ambao walienda nchini humo kwa ajili ya kutangaza dini, walirejea jana kwa ndege ya Shirika la Rwanda saa 9:55 mchana ambapo pia jana hiyohiyo waliondoka saa 12:00 kuelekea Zanzibar kwa ndege ya Shirika la Precision.

No comments

Powered by Blogger.