Header Ads

MSIMAMO WA UKAWA KWISHNEI, WABUNGE WAWILI WA CHADEMA WATINGA BUNGENI

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambaye pia ni mwanachama wa CHADEMA, Leticia Nyerere (kushoto) akitoka kujaza fomu ya mahudhurio ya vikao vya Bunge hilo huku akisindikizwa na mjumbe mwenzake, Steven Ngonyani

Kumekucha  katika Bunge Maalumu la Katiba, ambapo sasa baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamekiuka viapo na vitisho vya viongozi wao, kwa kuamua kutinga bungeni.

Katika mijadala mbalimbali, msemaji wa Ukawa ambaye pia ni Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amekuwa akisisitiza kwamba wajumbe wa Ukawa na hasa kutoka Chadema, hawatahudhuria Bunge Maalumu la Katiba.

Aidha, wiki iliyopita Chama cha Wananchi (CUF) kilisambaza waraka kwa vyombo vya habari, kuwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotoka katika chama hicho, kutohudhuria vikao vya Bunge hilo, vilivyoanza juzi.

Hata hivyo, katika kile kilichoonesha kutoungwa mkono kwa viongozi wa Ukawa ndani ya vyama vyao, baadhi ya wabunge waliozuiwa kushiriki vikao hivyo, wameonekana bungeni wakijisajili, kuashiria ushiriki wao bila kujali viapo na makatazo ya viongozi wao.

Leticia, Shibuda
Jana saa 5:55 asubuhi mjumbe wa bunge hilo, Leticia Nyerere ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Chadema, aliwasili kwenye viwanja vya bunge na kwenda moja kwa moja kwenye eneo la kujisajili na kukamilisha taratibu zinazotakiwa.

Hata hivyo, Leticia hakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari, wakati akienda kujiandikisha.

Hata wakati anatoka kukamilisha taratibu zinazotakiwa za kujisajili, pia alikataa kupigwa picha. “Unajua kwamba kunipiga picha bila idhini yangu ni ‘illegal (kinyume na sheria)? Sitaki,” alisema huku akielekea mlango wa kutokea, ambako alikutana na mjumbe mwingine wa bunge hilo, ambaye pia ni Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani (CCM), aliyekuwa akitoka pia kujisajili.

Ngonyani alisalimiana na Leticia na wakawa wanaongozana kutoka eneo la Bunge. Ngonyani alionekana mwenye furaha baada ya mjumbe mwenzake, kukamilisha taratibu za usajili.

Mapema juzi, wajumbe wengine wa Bunge hilo, Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda (Chadema) na Clara Mwatuka ambaye ni Mjumbe wa Viti Maalum kutoka CUF, nao walijisajili kushiriki vikao hivyo.

Wanaojishauri
Jana asubuhi pia zilikuwepo taarifa bungeni kwamba Mbunge wa Mpanda Kati, Said Arfi (Chadema), naye alijisajili. Lakini, akizungumza na mwandishi kwa simu, alisema alifika Dodoma, lakini hajaamua kama ajisajili ili ashiriki vikao au la.

“Sijajisajili bado, sio kweli, sijaamua nichukue huo uamuzi wa kushiriki au la, kama nikitaka kujisajili nitasema, ila kweli nipo Dodoma,” alisema Arfi ambaye alijiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema hivi karibuni.

Zitto
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), hivi karibuni aliibuka na kupingana na harakati za Ukawa.

Zitto alikaririwa akisema, hana uhakika wala hauamini Ukawa kama utakuwa umoja endelevu hadi kufikia Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, kwa sababu si mara ya kwanza vyama vya upinzani, kuungana na kugawanyika.

Zitto alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Power Breakfast, kinachorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds cha jijini Dar es Salaam, ambapo alisema Watanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi na si Katiba pekee.

Alisema siku zote Watanzania, wamekuwa wakipenda kuwa na upinzani imara, ambao watu wanaweka tofauti zao pembeni na kuungana dhidi ya chama ambacho kinaongoza, lakini haoni kama Ukawa utaendelea hadi kufikia kipindi cha Uchaguzi Mkuu.

Alisema hatua ya kusimama kwenye ajenda moja ya Katiba, haitausaidia umoja huo, kwani kipindi cha Uchaguzi Mkuu, kinakuwa na ajenda nyingi.

Alisema wananchi watapenda kusikia masuala ya kushughulikia rushwa, matumizi ya rasilimali, maji, umeme, afya na barabara.

“Mambo haya ndiyo yatakayowafanya wananchi waamue namna gani watakabidhi dhamana ya uongozi, si suala la Katiba pekee,” alisema Zitto.

Samuel Sitta  Juzi wakati akizungumza bungeni, Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alisema zaidi ya robo tatu ya wajumbe wa bunge hilo, walikuwa wamejiandikisha, ingawa hakutaja namba kamili. Pia, majina ya waliojiandikisha, hayatolewi kwa vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa Sitta, wajumbe wakishajisajli, fedha zao zinawekwa kwenye akaunti zao moja kwa moja kwa wale wenye akaunti ya Benki ya NMB. Wale ambao hawana akaunti NMB, wanachukua mkononi.

Aidha, katika mitandao mbalimbali, kulikuwa na taarifa kuwa karibu wajumbe 50 kutoka Ukawa, walikuwa wameshafika Dodoma, ingawa hawakuonekana katika viwanja vya Bunge.

Taarifa zingine zilieleza kuwa katika vyama hivyo, baadhi ya wabunge wanalalamikia viongozi wao, kususia Bunge Maalumu kutokana na ajenda zao binafsi, huku wao wakitakiwa na wapiga kura wao kuhudhuria bunge hilo.

Wajumbe waliojiundia kundi la Ukawa ambao wanatoka vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na CUF walisusia vikao vya bunge hilo Aprili mwaka huu, kwa kile walichodai halijadili Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba.

Bulembo  Wakati huohuo, Mjumbe wa Bunge hilo, Alhaji Abdallah Bulembo, alisema anaamini Katiba itapatikana na Ukawa watazidi kupasuka kadri muda unavyoenda.

“Tayari wameanza kujiandikisha, nasema watagawanyika siku si nyingi na Katiba itapatikana, hotuba ya Mwenyekiti (Sitta) juzi ilikuwa nzuri sana na imetoa mwelekeo wa mzuri,” alisema Bulembo, ambaye anatoka Kundi la Wajumbe 201, walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.

“Leo (jana) tumeanza kujadili rasimu kwenye kamati, tunajadili bila jazba, tunaenda vizuri na naamini mambo yatakamilika kama tunvyopanga." Mwandishi alimtafuta Msemaji wa CUF, lakini mara zote simu yake haikupatikana.

Baadaye, mwandishi alimpigia simu Jusa Ismail na kumuuliza juu ya tukio la Mbunge wa CUF, Clara Mwatuka kujisajili katika Bunge Maalum la Katiba, linaloendelea na vikao vyake huko Dodoma.

Jusa alijibu, “Siwezi kukisemea Chama. Mimi ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama, naomba umtafute Naibu Katibu Mkuu wa chama, Magdalena Sakaya, atakupa ufafanuzi”.

Ndipo, mwandishi alimpigia simu Sakaya, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum wa CUF. Lakini, mara zote simu yake ilikuwa haipatikani.

Kwa upande wa Chadema, mwandishi alimpigia simu Mkurugenzi wa Uenezi wa Chadema, John Mnyika ili atoe ufafanuzi wa juu wa wabunge wao wawili, Leticia Nyerere na John Shibuda, kujisajili kwenye Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.

Hata hivyo, simu zote mbili za Mnyika, hazikupatikana.

No comments

Powered by Blogger.