Header Ads

Wabunge na wasomi wazidi kumwandama Kitwanga

Siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kutimuliwa nafasi hiyo kwa ulevi, wabunge na wasomi wameendelea kumbana zaidi wakisema hatua hiyo ya Rais imechelewa.

Wapinzani wamekuwa wakimtaka Rais amuondoe kwenye nafasi hiyo kutokana na kuhusishwa na Kampuni ya Infosys ambayo ilitoa ushauri kwa Kampuni ya Lugumi Enterprises iliyopewa zabuni ya kufunga vifaa vya kuchukua alama za vidole (AFIS) katika vituo vya polisi.

Wakati wasomi wakisema hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema uamuzi huo ulikuwa sahihi na swali ambalo Kitwanga hakulijibu vizuri kutokana na hali ya ulevi, litapaswa kujibiwa upya baada ya wabunge kuomba mwongozo wa swali hilo.

Majaliwa alisema Rais ametengua uteuzi wa Kitwanga kuanzia juzi baada ya kuonekana amelewa wakati wa kazi.

“Na hili lilibainika pale alipokuwa akijibu maswali ya wizara yake...,” alisema Majaliwa.

Alisema uamuzi wa Rais Magufuli umefuata kanuni za utumishi wa umma ambazo zinakataza mtumishi kulewa akiwa kazini.

Ingawa Majaliwa hakutaja kanuni hiyo, Kifungu cha 34 cha Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002 pamoja na Kanuni ya 65 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003, kinasema, “Watumishi wa Umma wanapaswa kuepuka tabia ambayo inavunja heshima ya utumishi wao kwa umma hata wanapokuwa nje ya mahali pa kazi.

Tabia inayoweza kuvunja heshima hiyo inatajwa kuwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya, ulevi, kukopa kwa kiwango ambacho hawawezi kurejesha na mwenendo mbaya na kujihusisha na vitendo vyovyote viovu mbele ya jamii.

Bunge kuchukua hatua?

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah alipoulizwa adhabu ambazo mbunge anaweza kupata iwapo ataingia bungeni akiwa amelewa, alisema wanaoweza kujibu hilo ni Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni na Mnadhimu wa Serikali Bungeni, Jenister Mhagama.

Hata hivyo, Mhagama ambaye ni Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, alisema hawezi kueleza hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa kuwa tayari Rais ameshachukua uamuzi wa kutengua uteuzi huo.

“Ila Bunge lina taratibu na kanuni zake, nadhani Spika au katibu wa Bunge watakueleza vizuri,” alisema Mhagama.

Spika Job Ndugai hakupatikana kwenye simu, huku Naibu Spika simu yake iliita bila kupokewa.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Kanuni hazijaweka utaratibu wa mbunge anayeingia bungeni amelewa ila kuhusu suala la Kitwanga ni la nidhamu ya utumishi wa umma, labda kama atafanya jambo ambalo siyo la kawaida.”

Wabunge ‘wampa za uso’

Wabunge wa CCM na upinzani nao walitoa maoni kuhusu hatua hiyo wakisema ilikuwa haki kwa waziri kuachishwa kazi kwani alikuwa ametia aibu Serikali huku wakimpongeza Rais Magufuli kuwa yuko makini. Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alisema alichokifanya Magufuli ni kizuri na kwa sababu waziri huyo alishindwa kujiwajibisha mwenyewe.

Sakaya ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), alisema kitendo cha Dk Magufuli kumtimua mtu wake wa karibu, ni ishara tosha kuwa amedhamiria kuwasaidia wanyonge na kuwatahadharisha mawaziri wengine kuwa makini na kazi zao.

“Huyu waziri angeweza kujiwajibisha mwenyewe kutokana na makandokando yake, lakini akachelewa na sasa amekutana na mkono wa Rais kwa kuwa hataki uchafu, ni kweli jana (juzi) Kitwanga alikuwa amelewa wala siyo utani,” alisema Sakaya.

Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), alimpongeza Rais Magufuli kwa kuona jambo hilo akisema, haiwezekani kufanya kazi na watovu wa nidhamu hasa katika masuala ya ulevi.

Ndasa alisema kulewa ni sehemu ya utovu wa nidhamu lakini inakuwa shida zaidi pale viongozi wenye dhamana wanapolewa tena nyakati za kazi kwani inakuwa ni mfano mbaya, hivyo waziri huyo amevuna alichopanda.

Ali Saleh (Malindi – CUF) alisema Kitwanga alichelewa kuondolewa katika nafasi yake kwani alikuwa ni miongoni mwa majipu. Alisema waziri huyo alipaswa kuchunguzwa na Ikulu mapema baada ya kuanza kwa kelele za wapinzani, lakini watu wengi walishindwa kumpa Rais habari za ukweli kuhusu waziri wake. Alisema kutumbuliwa kwa Kitwanga kusitafsiriwe kwa mambo ya ulevi pekee, maana wakuu wa mikoa na wilaya wataanza kufanya hivyo kwa uonevu kwa watu ambao watakuwa wamewanyima hata pombe vilabuni.

Joel Mwaka (Chilonwa – CCM) alimpongeza Rais Magufuli kuwa ni mtu anayeyaishi yale anayoahidi na hivyo kuwapa nafasi kubwa Watanzania na hasa wa chini huku akitahadharisha viongozi kuacha kuwadharau watu wa hali ya chini.

Suzan Kiwanga (Mlimba – Chadema) aliyezusha sakata hilo, aliwalaumu wasaidizi wa Kitwanga pamoja na dereva wake kwamba walishindwa kumshauri asiingie bungeni.

“Hakuwa katika hali ya kawaida, alilewa sana jamani hadi akashindwa kujibu swali, ningeshauri Rais aangalie sana kwa mawaziri wake kwani wengi wanaonekana kulewa hata madaraka na kujibu maswali kwa nyodo,” alisema Kiwanga.

Mitandaoni

Jana kutwa nzima, mitandao ya kijamii ilitawaliwa na taarifa za kutimuliwa kwa Kitwanga ikiambatana na video yake wakati akijibu swali bungeni katika hali ya ulevi.

Vilevile, ilisambaa video ya Rais Magufuli wakati wa kampeni akimnadi mbunge huyo Misungwi mkoani Mwanza, huku akieleza bayana kuwa ni rafiki yake wa karibu ambaye walisoma wote chuo kikuu.

Pia, kulikuwa na video nyingine iliyosambaa ikimuonyesha Kitwanga akifurahi pamoja na Dk Magufuli huku akimpigapiga mabegani walipokuwa wakijadili kuhusu joto linalohitajika kuyeyusha madini ambako baada ya maelezo marefu, Kitwanga anasikika akimwambia Magufuli, “chukua fomu basi.” Naye akajibu “fomu ya nini (vicheko), hebu nieleze... mimi watu watalimia meno.”



Siri ya Kitwanga

Mmoja wa wabunge wa karibu na Kitwanga kutoka Kanda ya Ziwa ambaye hakupenda kutaja jina lake, alitoa sababu za kiongozi huyo kulewa akisema, inatokana na mawazo mengi aliyonayo ya kufiwa na kijana wake wa kiume.

Mbunge huyo alisema Kitwanga alikuwa na mtoto mmoja wa kiume ambaye alimtegemea lakini tangu alipofariki hayuko kwenye hali nzuri na ndiyo maana amekuwa akinywa pombe kupita kiasi.



Wasomi wamwandama

Kama ilivyokuwa kwa wabunge wasomi na wachambuzi wa siasa wamesema Kitwanga alitakiwa kuondolewa madarakani mapema, kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Lugumi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema ni aibu kwa waziri aliyetakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii, kuingia bungeni akiwa amelewa. Alisema licha ya tuhuma za ulevi, aliandamwa na kashfa nyingine ikiwamo ya Lugumi jambo ambalo lilimuondolewa uaminifu kwenye jamii na alistahili kuondoka madarakani.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema kwa kuwa waziri alikuwa na kashfa nyingi, isingekuwa rahisi kwa Rais Magufuli kuendelea kumuacha kwa sababu tayari alikosa sifa za uongozi.

“Kosa la ulevi ambalo lingeweza kupelekwa kwenye kamati ya nidhamu ya Bunge ndilo ambalo limemuondoa, maana yake isingekuwa rahisi kwa Rais kumuondoa kwa kashfa ya Lugumi ambayo, bado ni kizungumkuti,” alisema.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Kitila Mkumbo alisema kiuhalisia, Kitwanga hakuwa na sifa za kuwa waziri kwenye wizara nyeti, kutokana na sifa yake ya ulevi.

“Ukiniuliza kama Kitwanga alikuwa na sifa za kushikilia wadhifa huo, nitakukatalia kwa sababu hata kwenye kampeni zake kuna wakati alienda akiwa amelewa, hivyo hakustahili kupewa wizara hiyo nyeti,” alisema.

Mchambuzi wa siasa mkazi wa Iringa, Dk Frank John alisema ni wakati wa viongozi waliopo madarakani kuheshimu nafasi zao kwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema: “Eti wanadai ametumbuliwa sababu ya ulevi, hebu jiulize Waziri wa Mambo ya Ndani ana wasaidizi, ana mlinzi ana katibu ana dereva, huyu mtu aliyelewa kiasi hicho katibu alishindwa kumwambia maana kazi yao ni kumsaidia waziri asifanye mambo ya aibu. Sasa utawala uliofitinika hauwezi kusimama kamwe kuongoza taifa,” alisema Lema.

Waziri wa Zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha alimpa pole Kitwaga akisema, hata yeye alikuwa anakunywa ndovu akiwa waziri lakini hakuwahi kutimuliwa.

“Namuonea huruma Kitwanga kwa sababu alikuwa haijui CCM, kama ni pombe mbona hata mimi nilikuwa nakunywa ndovu, nakijua chama hicho nilianzia chipukizi, hata umoja wa vijana, lakini niliamua kutoka,” alisema Masha.

No comments

Powered by Blogger.