Header Ads

Picha za ngono mitandaoni zinavyowaathiri vijana

Tuna msemo usemao shilingi ina pande mbili, kwa maana ya kwamba katika kila kitu kuna uzuri na ubaya wake. Ni sawa na teknolojia, tunaamini kuwa imeleta mambo mengi mazuri lakini pia imechangia kwa kiasi kikubwa kueneza mambo mabaya ikiwemo picha na video za ngono. Mtandao wa internet sasa umekuwa mwalimu mkubwa wa kufundisha masuala ya kujamiiana kwa vijana wengi. Hili ni tatizo kubwa kwasababu unatoa mtazamo mbaya wa kujamiiana na vilevile mtazamo mbaya wa uhusiano wa binadamu, ambapo kwa kiasi kikubwa unachangia ukatili dhidi ya wanawake na kuhamasisha vitendo vibaya.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali duniani hivi sasa picha na video za ngono zinapatikana zaidi kwenye mtandao ikilinganishwa na huko nyuma, ambapo watu wanaweza kupata picha hizo kwa kutumia vifaa mbalimbali popote pale walipo, na wakati wowote wanaotaka iwe usiku au mchana, lakini upatikanaji wa picha hizo kwa kweli unaweza kutuathiri vibaya, hususan zikiwa zinaangaliwa na vijana. Tuchukulie mfano nchini Australia takwimu zinaonesha kuwa vijana wa kike na kiume wanaongalia picha hizo kutoka umri wa miaka 9 hadi 16 basi wanafikia asilimia 28. Huku nchini Uingereza moja ya kumi ya watoto kati ya umri wa miaka 12 na 13 wanahofiwa kuwa waathirika wa picha hizo. Na hata Marekani nako takwimu zinaonesha asilmia 42 ya watoto kati ya umri wa miaka 10 na 17 wanaangalia kwa makusudi au kwa bahati mbaya.

Lakini huo ni mfano wa nchi za Ulaya tukirudi hapa China, tukiangalia ama kweli suala hili la kuangalia picha za kujamiiana kwenye mtandao linapendwa na vijana wote? Mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari hapa mjini Beijing anaona kuwa kupata video za kujamiina ni jambo ambalo ni la kawaida kwa wanafunzi hata hivyo anaona sio vizuri kwa vijana kuangalia picha hizo kwenye mtandao wa Internet. Anasema:

"Labda wanapeana, au download kwenye mtandao wa internet. Kuna njia nyingi za kuzipata picha na video hizo, na ziko nyingi kwenye mtandao. Kwetu sisi wanafunzi wa sekondari, tukizitaka tunaweza kuzipata. Hili ni jambo baya sana."

Kwa kweli kama alivyosema huyo mwanafunzi hili ni jambo rahisi mno kwa wanafunzi kulipata, ingawa serikali inachukua hatua kali lakini bado watengenezaji wanaendelea kusambaza kwa njia za siri, bila kujali nani atakayeathirika zaidi. Ni vizuri hao wahusika wangekuwa wanafanya kama vile unavyokwenda dukani kununua video za aina hiyo na kuambiwa utoe uthibitisho wa umri wako. Lakini wazazi nao kwa upande fulani wanachangia kwani wanawaacha watoto wao wanaingia kwenye tovuti zisizofaa bila ya kuwakataza au kuwafuatilia. Ndio, inaweza kuwa wakati anapoangalia usijue lakini mzazi unatakiwa uwe na utaratibu wa kuangalia laptopu ama kompyuta ya mtoto wako kila baada ya kipindi fulani ama mara mbili kwa wiki kuhakikisha kuwa hangalii tovuti zisizofaa.

Tunajua kwamba China imepiga marufuku picha na video za kujamiiana tangu iasisiwe mwaka 1949. Mtu yeyote anayetengeneza, kusambaza, au kununua vitabu, magazeti au video zinazohusiana na mambo hayo anapewa adhabu. Lakini hivi leo, kusambaza picha na video hivyo kupitia mtandao ni suala jipya.

Serikali ya China imeamua kuchukua hatua kali dhidi ya wale wanaohusika kuweka picha za kujamiiana kwenye mtandao ili kuhakikisha maadili ya jamii hayaporomoki na pia kulinda afya za kiakili za watoto wa kike na kiume. Tumepata habari kuwa, wiki iliyopita, ofisi husika ya serikali ya China iliitisha mkutano na wadau kutoka tovuti za mtandao zinazotumiwa kwa wingi na watu wa China, ikisisitiza kuwa, vitendo vya kusambaza picha na video vya ngono kwenye internet vimedhuru kwa kiasi kikubwa jamii, hususan afya ya kimwili na kisaikolojia wa vijana, wazazi na walimu wana wasiwasi mkubwa. Ofisi hiyo imesema, ni lazima kupambana na tovuti zinazotambulika kujihusisha na vitendo hivyo. Ofisi hiyo pia ilitangaza matokeo ya zoezi liitwalo "kusafisha mtandao mwaka 2015", ambapo baadhi ya tovuti zilihukumiwa, baadhi kutozwa faini, na baadhi kuagizwa kujisahihisha.

Shirikisho la mtandao wa internet mkoani Guizhou, kusini magharibi mwa China na kupendekeza software moja bila malipo, wazazi wanaweza kutumia software hii ili kuchuja habari zisizo za kweli na habari mbaya za ugono na ukatili. Na baadhi ya wanawake mjini Shi Jiazhuang kaskazini mwa China nao pia wameanzisha tovuti za kupinga video za ngono kwenye mtandao, na kutoa ripoti kwa polisi tovuti zaidi ya elfu 4 zinazoonesha video na picha za ngono.

Na mfano mzuri wa adhabu hizo ni pale mwaka 2005 mwanzilishi wa mtandao mkubwa wa Video za kujamiiana alihukumiwa kifungo cha maisha jela. Lakini mbali na hapo Studio au watengenezaji filamu wanaokamatwa wakitengeneza filamu za aina hiyo wanaweza kupoteza leseni ya kutengeneza filamu kabisa.

Wataalamu mbalimbali wanaona kuwa athari mbaya za kiafya zinazotokana na kuangalia video za kujamiana kwenye mtandao zaidi zipo kwenye sehemu mbili. Kwanza ni tabia za ngono zinazoweza kuongeza hatari ya maambukizi mbalimbali ikiwemo Virusi vya Ukimwi, kaswende, kisonono n.k. Na sehemu ya pili inahusiana na kuondoa mtazamo halisi, hususan kama video inayoangaliwa inaonesha tendo linalofanyika kwa fujo. Katika baadhi ya kesi picha hizi zinawafanya vijana kuamini kuwa tabia za kujamiiana zisizofaa, kama vile vurugu, ukali au kufanya tendo hilo bila ya ridhaa ya mwanamke ni mambo ya kawaida na yanayokubalika. Kuhusu athari za kuangalia video za ngono kwa saikolojia za vijana, mtaalamu anayeshughulikia mambo ya vijana Guo Haiyan anaeleza:

"Hivi sasa, kujamiiana kabla ya ndoa ni jambo la kawaida katika jamii ya wanafunzi wa vyuo vikuu na vijana, jambo hili hata wao wenyewe hawafichi kusema. Naona wameathiriwa vibaya katika mazingira ya utamaduni mbaya. Kama wanapokea maelekezo mazuri na mawazo mazuri, wasingekuwa na mwelekeo huu mbaya."

Na katika nchi za Afrika video ama picha za ngono zinaangaliwa sana tu na vijana kwenye mitandao. Na hivi karibu imezuka tabia ambayo ni mbaya sana dhidi ya watu mashuhuri hususan wa Afrika Mashariki na Magharibi kuvujishiwa picha ama video zinazoonesha wakifanya ngono. Na ubaya wenyewe ni kwamba huwekwa kwenye mitandao ya kawaida ambayo mtu yeyote anaweza kuangalia.

Watoto hawapaswi kuruhusiwa kuangalia picha hizi na serikali zinapaswa kuchukua hatua kali kuzuia mitandao inayoonesha picha ama video hizo. Kwani kama hatua hazikuchukuliwa na mapema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ambavyo tumekuwa tukivipiga vita kila siku vitaendelea kuwepo kutokana na vijana hao kupata mitazamo isiyo sahihi kuhusu kujamiiana, pia Waswahili wanasema usipojenga ufa utajenga ukuta kwa maana ya kwamba tusisubiri hadi watoto waharibike ndio hatua zichukuliwe, ni vyema wakiwahiwa mapema

No comments

Powered by Blogger.