Header Ads

Agizo la Waziri mkuu kwa waziri wa kilimo......

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. Mwigulu Nchemba afanye mapitio ya vitalu vyote vilivyoko katika ranchi ya Kitengule wilayani Karagwe na kujua nani anamiliki kitalu kipi na kama hajaendeleza kwa mujibu wa makubaliano ni vema akanyang’anywa.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi jioni (Jumatatu, Machi 14, 2016) alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya Kihanga wilayani Karagwe ambapo aliitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ifanye mapitio katika vitalu vyote na kuangalia wamiliki ni akina nani na kukagua vibali vyao.

Pia aliagiza wavamizi wote kuondoka katika pori la akiba la Kimisi lililoko wilayani Karagwe ambao wanatoka nchi jirani na kuwataka warudi makwao na wakaanze upya kutuma maombi ya kuja kuishi nchini.

“Lazima tulinde nchi hii kwa pamoja. Pamoja na kuwa tunatambua ujirani uliopo na uanachama wa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki bado kuna taratibu na kanuni ambazo ni lazima zifuatwe. Tunao utaratibu wa kutoa kibali cha muda usiozidi miezi sita… hawezi mtu kuja akaamua kukaa tu bila kibali na wala Mtanzania huwezi kwenda nchi jirani ukaamua kukaa tu bila kufuata taratibu,” alisisitiza.

Akizungumzia migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji iliyokithiri mkoani Kagera, Waziri Mkuu alisema inasababishwa na viongozi na wananchi kuruhusu watu wa mataifa mengine kuingia nchini bila ya kufuata utaratibu, ambapo aliwataka wabadilike na waache tabia hiyo.

“WanaKaragwe mmeamua kuruhusu watu wa mataifa mengine waje kufaidi rasilmali zetu. Hapa kuna Warundi na Wanyarwanda. Je wamefikaje kama siyo ninyi kuwaruhusu?" alihoji.

“Lazima tushirikiane kulinda mipaka, nimeangalia mpaka wa nchi yetu kule Misenyi naona mambo ni hovyo hovyo tu. Vitalu vingi vinamilikiwa na wageni, kuanzia namba 1,5,7,9,10,11 na 12 na wengine hawajaendeleza kabisa. Kwa mfano kitalu namba tano kinatumiwa kulima bangi, Wizara mnasubiri nini kuwanyang’anya na kukirudisha kwa Watanzania?”

“Wizara mfanye mapitio katika vitalu vyote vilivyo pembezoni mwa vijiji. Angalieni nani anamiliki, amepewa kwa kazi ipi na kama kama hajafanya kitu chochote  basi ni vema wakabidhiwe Watanzania wenye mifugo ili wavitumie kunenepesha mifugo yao,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.

Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu alisema kuna kitalu kimoja kina hekta 36,000 na ilikubalika kuwa kitajengwa kiwanda cha kusindika nyama nyama ya ng’ombe lakini hata hivyo hakijafanyika kitu. “Wizara mkafanye mapitio mumpunguzie eneo huyo mmiliki ili wafugaji wa Karagwe wafuge na kunenepesha ng’ombe wao na kisha kuuza katika kiwanda hicho.

Waziri Mwigulu ambaye ameambatana Waziri Mkuu katika ziara hii ya siku tatu, ameenda Karagwe leo hii kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu wakati Waziri Mkuu akielekea wilaya ya Ngara

IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, MACHI 15, 2016.

No comments

Powered by Blogger.