Header Ads

Waziri wa nchi ofisi ya rais akichafua Zanzibar, Aelezea mishahara ya mawaziri wa CUF Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Machano Othman Said, amesema kitendo cha Mawaziri wa CUF wanaounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kujivua nyadhifa zao bila kumwandikia barua ya kujiuzulu rais, ni sawa na kuwadanganya Wananchi wa Zanzibar.

Tamko hilo alilitoa jana akiwa ofisini kwake Forodhani Zanzibar, wakati akifanya mahojiano maalum na Nipashe juu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutimiza miaka mitano.

Alisema waziri anateuliwa na rais na katika mazingira yoyote kama waliamua kujivua nyadhifa zao, walitakiwa kuandika barua za kujiuzulu ili stahiki zao zipate kusitishwa kwa mujibu wa sheria.

Waziri huyo alisema kitendo cha kuendelea kulipwa stahiki zao bila ya kuonekana kazini hakikubaliki katika misingi ya utawala bora na kwamba ni kutumia vibaya fedha za umma.

“Kujiuzulu waziri siyo kurejesha gari na mali za serikali, unatakiwa kuandika barua ya kujiuzulu kwa rais ili stahiki zako za malipo ya kila mwezi zisitishwe.”alisema Waziri Machano.

Alisema haikuwa muafaka kwa Mawaziri wa CUF kujivua nyadhifa zao kwa kuondoka kimya kimya bila kuandika barua kwa rais, hivyo kusababisha Wizara ya Fedha kuendelea kuwalipa stahiki zao kila mwezi licha ya kutokuonekana kazini.

Waziri Machano alisema  msimamo uliyochukuliwa na Mawaziri wa CUF unaleta matabaka na kuchonganisha watu na serikali yao kinyume cha malengo ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2009.

Alisema ukiondoa misukosuko ya uchaguzi, serikali ya pamoja imeweza kufanikiwa kuleta hali ya utulivu wa kisiasa na milango ya misaada kufunguka kwa wahisani hatua ambayo imesaidia kasi ya maendeleo kuanza kuonekana katika sekta ya miundombinu huduma za umeme na mabadiliko makubwa ya bei ya zao la karafuu kwa wakulima visiwani hapa.

Aidha, Waziri Machano alisema mkwamo wa uchaguzi usiwe chanzo cha kuvuruga msingi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu madhara yake ni makubwa na yataathiri mafanikio yaliyokuwa yameanza kupatikana Visiwa vya Unguja na Pemba.

Waziri Machano alisema Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein bado ni rais halali kwa mujibu wa Kifungu cha 28(1) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 ataendelea kuwa rais mpaka rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar pamoja na Baraza lake la Mawaziri visiwani hapa.

Hata hivyo, Mawaziri wa CUF saba na Manaibu wake watatu wakiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakar, wamesema serikali ya awamu ya saba imefikisha kikomo cha kubakia madarakani Novemba 2, mwaka huu kwa mujibu wa Kifungu cha 289( 2) cha Katiba ya Zanzibar kuwa rais ataacha madaraka yake baada ya kumaliza miaka mitano kuanzia tarehe ya kuapishwa na kula kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar.

Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, alisema wameondoka bila ya kuandika barua kwa sababu rais amemaliza muda wake na hatua ya kumuandikia barua ni sawa na kubariki kuendelea kwake kubakia katika wadhifa huo.

Mbarouk alisema wameanza kuwasiliana na wanashaeria ili waweze kurejesha mishahara ambayo wamekuwa wakilipwa kila mwezi bila ya kufanya kazi baada ya kujivua nyadhifa zao na kupata baraka za chama kuanzia Novemba mwaka huu.

Mgogoro wa ukomo wa Serikali ya awamu ya saba Zanzibar umeibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 kwa madai ulitawaliwa na vitendo vya udanganyifu na kuwataka wananchi kusubiri kufanyika uchaguzi wa marejeo.

No comments

Powered by Blogger.