Header Ads

Hizi Ndio njia 9 za ukwepaji kodi bandarini Dar

Wakati Serikali ikikunjua makucha yake dhidi ya wote waliohusika katika kashfa ya kupitisha makontena 349 kwenye Bandari ya Dar es Salaam bila ya kuyalipia kodi, imefahamika kuwa idadi hiyo ya makontena ni sehemu ndogo tu ya mamia ya mizigo yanayovushwa kinyemela kila uchao na kuikosesha serikali mabilioni ya fedha.

Kuanzia mwishoni mwa wiki, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli imekuwa ikichukua hatua kadhaa za kukomesha ukwepaji kodi katika Bandari hiyo inayotegemewa zaidi kwa mapato nchini. Hadi sasa, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), Rished Bade, amesimamishwa kazi na kushikiliwa polisi kuhusiana na taarifa za serikali kukosa mapato takriban Sh. bilioni 80 kutokana na makontena hayo (349) kupitishwa bila ya kulipiwa kodi. Kadhalika, vigogo wengine kadhaa wa TRA wamesimamishwa kazi pia na kushikiliwa na polisi wakati uchunguzi zaidi kuhusiana na kashfa hiyo ukiendelea.

Hata hivyo, wakati serikali ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu wake, Kassim Majaliwa, ikiendelea kutafuta suluhu ya kudumu kuhusiana na ukwepaji kodi, Nipashe imebaini kuwa kazi hiyo siyo lelemama kwani zipo njia zaidi ya tisa zinazotumiwa kukwepa kodi katika Bandari ya Dar es Salaam.

Uchunguzi wa Nipashe uliohusisha mahojiano na vyanzo mbalimbali umebaini kuwa wanaofanikisha ukwepaji wa kodi hushirikiana kupitia mtandao mpana unaohusisha wafanyabiashara wasio waaminifu, maafisa wa TRA, watumishi wa Bandari, wamiliki wa kampuni za usafirishaji na uondoaji mizigo, maafisa wa bandari kavu, maafisa wa benki zinazopokea malipo na pia baadhi ya askari.

Chanzo kimeiambia Nipashe kuwa viongozi wa juu wa taasisi mbalimbali zinazoshughulikia uondoaji mizigo bandarini jijini Dar es Salaam wamejiundia mitandao mipana inayoingiza mamilioni kila uchao na hivyo vita iliyoanzishwa na serikali ya Dk. Magufuli inapaswa kuwa endelevu ili kuleta mafanikio.

“Zipo njia nyingi zinazotumiwa na watu hawa kufanikisha hujuma hizi kwa manufaa binafsi. Baadhi ya wale wanaoshiriki mchezo huu ni watu wazito na kwa muda mrefu wamejijengea ushawishi mkubwa serikalini na hivyo vita hii iliyoanzishwa na Dk. Magufuli na Waziri Mkuu wake siyo ndogo… ni kazi kubwa na kila mmoja anapaswa kuwaunga mkono, “chanzo kingine kimeiambia Nipashe.

NJIA 9 ZA UKWEPAJI KODI BANDARINI DAR
 
Vyanzo vimeiambia Nipashe kuwa maeneo yanayotumiwa kufanikisha ukwepaji wa kodi yapo mengi, lakini makubwa yanayofahamika zaidi bandarini hapo ni tisa. 

 Mosi, ni kupitia mwanya utokanao na mfumo wa zamani wa malipo usiohusisha ule wa sasa wa kielektroniki, maarufu kama ‘E-Payment’. Kwamba, wafanyabiashara wengi hutumia mfumo huo wa zamani unaohusisha matumizi ya karatasi zilizojazwa kwa mkono na hivyo kuwezesha ujanja wa kubadili taarifa kwa manufaa ya mitandao ya wakwepaji wa kodi.

 “Tatizo lililopo ni kwamba mfumo wa E-Payment ni mpya (umeanza Julai) na umefungwa kwenye benki moja tu iliyopo ndani ya eneo la Bandari… ule wa zamani unaendelea kutumiwa na wajanja hucheza na maandishi ya kujaza kwa mkono kuhujumu mapato ya serikali,” chanzo kimeeleza.

Njia ya pili ya kuhujumu mapato bandarini hapo, imetajwa kuwa ni ya kushirikiana na maafisa wa benki. Hii ina uhusiano mkubwa na njia ya kwanza inayohusisha matumizi ya mfumo wa malipo wa zamani usiokuwa wa kielektroniki. Mfanyabiashara anaweza kuandikiwa kodi sahihi anayotakiwa kulipa, lakini anashirikiana na wafanyakazi wa benki anayokwenda kuweka fedha kwa kuhakikisha kuwa baada ya kufanikiwa kuondoa kontena bandarini, maafisa wa benki husika husitisha malipo hayo kwa kuondoa fedha husika kwa madai kuwa fedha ziliingizwa kwenye akaunti husika kimakosa.

“Huwa kuna ushirikiano wa karibu kati ya maafisa wa benki na mfanyabiashara husika. Baada ya kontena kutolewa bandarini, hamisho la fedha (transaction) huondolewa katika mfumo kwa maelezo kuwa halikuwa sahihi,” chanzo kimedai, huku kikisisitiza kuwa ushirikiano huo huhusisha pia watu wa Bandari na TRA ambao mwishowe hugawana malipo kadri wanavyokubaliana.

Tatu, ni mwanya wa uvushaji wa makontena yenyewe yasiyolipiwa ushuru kupitia mageti maalum yanayofahamika kwa kazi hiyo, hasa geti Namba 3 ambalo chanzo kimedai ndilo linaongoza kupitisha mizigo ya ‘dili’.

“Kwa ujumla yapo mageti matano ya kupitisha bidhaa mbalimbali, baadhi yakiwa ni ya kupitihia mafuta, nafaka na magari. Hili Namba 3 ndiyo hutumika kupitisha makontena ya bidhaa zenye thamani kubwa na wengi wasiolipa kodi hulitumia hili,” chanzo kilieleza kabla ya kufafanua kuwa awali, hilo geti Namba 3 halikuwa na mfumo wowote wa kuangalia kama kontena husika limelipiwa au la na ndiyo maana lilikuwa likitumika zaidi kupitisha makontena yasiyolipiwa kodi.

Njia ya nne ya kuhujumu kodi ya mapato ni ya kuwatumia watu wanaoendesha bandari kavu (ICD’s). Inaelezwa kuwa hivi sasa kuna bandari kavu 12, ambazo kila meli inapoingia hujulikana kila mzigo husika unapelekwa kwenye bandari ipi kati ya hizo. Hata hivyo, inaelezwa kuwa kinachofanyika ni kwa baadhi ya makontena yanayotolewa bandarini ili yapelekwe bandari kavu kabla ya kukombolewa na wahusika huishia kupelekwa kwa wafanyabiashara wenye makontena na hivyo kuikosesha mapato serikali.

“Awali kwenye ICD’s kulikuwa na askari wa mmiliki wa ICD’s na siyo wa TPA… huyu alikuwa akiangalia malipo ya bosi wake tu ambayo ni gharama za kuhifadhi mzigo na hivyo TPA na TRA huambulia patupu,” chanzi kimeeleza, kikiongeza kuwa hivi sasa walau kuna nafuu kwani kwenye ICD’s kuna walinzi wa TPA lakini hilo limefanyika baada ya watu kuwa tayari wameshaiba sana.

Njia ya tano inayotumiwa kukwepa kodi ni ya kubadili taarifa, hasa kupitia watu wenye wajibu wa kufanya tathmini. Kwamba, badala ya mzigo kukadirwaa kodi kwa kiwango sahihi, wahusika ambao zaidi huwa ni watu wa TRA hukadiria fedha kidogo baada ya kujihakikishia kuwa nao wanapewa mgawo na wafanyabiashara.

“Hapo utakuta kontena la kodi ya milioni 80, mteja anaambiwa alipe milioni 40 tu … na wakati mwingine kiasi hicho pia hakiandikwi balki huandikwa cha chini zaidi kama milioni 5 tu…hii ni njia nyingine inayoligharimu taifa mabilioni ya fedha,” chanzo kimeeleza.

Chanzo kimeeleza zaidi kuwa njia ya sita inayofanikisha ukwepaji kodi ni mtandao mpana wa baadhi ya vigogo wa maeneo mbalimbali Bandarini na TRA, ambao hawa huhakikisha kuwa wanakuwa na timu ya vijana wao wa kazi karibu katika kila eneo ili kufanikisha mipango yao.

“Hii ndiyo njia kubwa ya hujuma. Kama utakumbuka aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisambaratisha baadhi ya mitandao kwa kuwagusa vigogo 27…  ile ilikuwa kuvunja mtandao uliokuwapo. Hilo lilisaidia kiasi, lakini sasa ipo pia mitandao mingine ambayo uchunguzi ukifanyika utabaini kuwa mambo yameanza kurudi kama zamani,” imeelezwa.

Njia ya saba ya ukwepaji kodi ni kwa baadhi ya vigogo wa Bandari na TRA kuanzisha kampuni zao za uondoaji mizigo bandarini. Inaelezwa kuwa hizi hutumiwa sana kufanikisha ‘dili’ za ukwepaji kodi na ndiyo maana haishangazi kusikia kuwa kuna makontena zaidi ya 300 hayaonekani kwenye kumbukumbu za TRA.

Chanzo kimeeleza zaidi kuwa njia ya nane ya ukwepaji kodi ni kuonyesha kuwa kontena linapelekwa nje ya nchi, kwa mfano Malawi, wakati ukweli ni kwamba huishia hapahapa nchini.

“Utakuta kontena linadaiwa kupelekwa Malawi, lakini linachukuliwa na gari kukuu linaloonekana wazi kuwa haliwezi kufika hata Kibaha… njia hii pia hutumiwa sana kuikosesha serikali mapato,” chanzo kingine kiliiambia Nipashe.

Kadhalika, chanzo kiliitaja njia ya nane ya ukwepaji kodi kuwa ni ucheleweshaji wa makusudi wa utoaji makontena. Kwamba, mteja anapotaka kutoa mzigo wake kwa kufuata njia halali zilizopo, huishia kuzungushwa kila uchao ili akubali kutoa rushwa na mwishowe kulipishwa kiwango pungufu cha kodi au kulipa fedha zisizoingia kabisa kwenye mikono ya TRA.

Njia ya tisa, kwa mujibu wa chanzo chetu, ni ubabaishaji unaofanyika katika kuorodhesha idadi ya makontena inayotolewa bandarini kwenda kwenye bandari kavu. Hapa, kama makontena yanayotolewa ni 12, basi huandikwa kuwa ni 10 na mengine mawili huishia kunodolewa bila ya kuwa na kumbukumbu zake kwa ajili ya kulipiwa kodi.

Pamoja na kuwapo kwa njia zote hizo, chanzo kimedai kuwa sababu kubwa ya kufanikiwa kwa ukwepaji kodi ni mtandao mpana unaoundwa na vigogo mbalimbali na ndiyo maana taarifa mbalimbali za wakaguzi wa ndani na wa nje katika Bandari ya Dar es Salaam huishia kubaki kwenye makabrasha bila ya kuwapo kwa utekelezaji wowote wa vitendo juu ya yale yanayopendekezwa na wataalamu.

WAFANYABIASHARA WAFICHUA ZAIDI

Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabishara Tanzania, Johnson Minja, alisema suala la serikali kupoteza mapato makubwa bandarini lilikuwa kilio chao cha muda mrefu na hivyo wanafurahi kuona kuwa sasa, chini ya Rais Magufuli, serikali imeanza kushughulikia tatizo la hujuma ya mapato ya serikali kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Alisema kilio chao kikubwa kilikuwa ni kuiomba serikali kuweka bei elekezi ya kutoa kontena bandarini kulingana na bidhaa badala ya kuwa na bei holela ambayo mwishowe wakubwa wengi walitumia mitandao yao kulipa kidogo huku wengi walio na mitaji midogo wakiumia kwa kutozwa kodi kubwa ili kufidia kiwango kisicholipwa na wakubwa.

BEI ELEKEZI YA SASA
Minja alisema waliamua kwa pamoja kila kontena la futi 40 la mzigo wa nguo litozwe kodi ya Sh. milioni 25 bandarini huku kwa vifaa vya ujenzi walipitisha bei elekezi kuwa ni Sh. milioni 27 kwa kontena moja.

“Kontena la vifaa vya umeme lenye ukubwa wa futi 40 ni Sh. milioni 30 huku kontena la vitenge la futi 40 likitozwa kodi ya Sh. milioni 40,” alisema, akiongeza kuwa bei hiyo elekezi imeanza Novemba baada ya Magufuli kushinda urais Oktoba 25.

Minja alisema awali vigogo na maofisa wa TRA walikuwa wakihusika kupitisha mizigo bila kutoza kodi au kutoza kidogo kwa baadhi ya watu.

POLISI
Idadi ya watu waliokamatwa kutokana na kuhusishwa na hujuma ya ukwepaji kodi kutokana na makontena 349 yaliyopitishwa bandarini kinyemela imezidi kuongezeka baada ya watu wengine kadhaa kukamatwa jana na kuwekwa mbaroni.

Inaelezwa kuwa kati ya wale waliokamatwa jana, ni pamoja na baadhi ya wafanyabiashara na pia vigogo zaidi wa TRA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Luca Mkondya, alisema kuwa suala hilo ni nyeti na linahitaji upelelezi wa kina na hivyo, licha ya kukiri kuwa wamewakamata watu wengine zaidi jana, lakini hakuwa tayari kutaja idadi ya watuhumiwa hao waliowaweka mbaroni wala majina yao.

Badala yake, Kamanda Mkondya alisema alisema kumalizika kwa upepelezi kunategemeana na jinsi watakavyopokea ushahidi kwa wakati na baada ya hapo hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa.

Aidha, Kamanda Mkondya hakutaka pia kuzungumzia kuhusu kuwapo kwa dhamana kwa watu hao waliowashikilia, wakiwamo vigogo wa TRA.
Alipioulizwa, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova, alisema atatoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na watu waliokamatwa juu ya makontena yasiyolipiwa kodi bandarini leo.

“Kila kitu ni kesho (leo)… nitaitisha press conference na kueleza kwa kina,” alisema Kamanda Kova.
Credit: Nipashe

No comments

Powered by Blogger.