Header Ads

Baada ya Dc Makonda kuwaweka Rumande maofisa ardhi sasa ni kazi tu

Baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuwaweka rumande kwa takribani saa 6 maofisa wa ardhi wa Manispaa ya Kinondoni waliochelewa kuhudhuria kikao cha utatuzi wa migogoro kwenye Kata ya Wazo jana, mapema leo maofisa hao wameonekana kuanza kazi yao kwa kasi baada ya kufika saa mbili kabla ya kikao kuanza.

Akizungumza kwenye kikao cha pili kilichofanyika katika kata ya Wazo kijiji cha Nyakasangwe nje kidogo ya jiji la Dar, baada ya kile cha jana kuahirishwa kutokana na uchelewaji wa maofisa hao, Makonda amesema kuwa hana tatizo na maofisa wake na kuwataka waelewe kuwa alilazimika kufanya hivyo kutokana na kasi yake ya utendaji na kuwasifu kwa kuwa wavumilivu na kuwahi siku ya leo.

Mbali na hayo Makonda amesema kuwa ameunda kamati inayowahusisha wenyeviti saba na wajumbe kumi na mbili wa kata nzima ya Wazo ambao watakuwa na kazi za kutambua ukubwa maeneo yenye migogoro, kutazama uhalali wa umiliki wa maeneo husika na kuwapa hatimiliki waliothibitishwa kuwa ni wamiliki halali wa maeneo hayo.

Aidha Makonda amewatoa hofu wakazi wa maeneo hayo waliofurika kutaka kujua hatma ya viwanja vyao,akisema kuwa anatambua uwepo wa watu wanaomiliki viwanja hivyo kwa njia ya kurithishwa, kupewa kama zawadi na wengine kuuziwa kwa kutumia kanuni za kijiji na kuongeza kuwa bila kujali wananchi wote waliopeleka malalamiko yao watapata haki zao stahiki.

Alifafanua kuwa anatarajia kuimaliza kabisa migogoro hiyo iliyogharimu maisha ya watu saba huku wengine wakipoteza makazi yao na kuwataka wananchi kuwapa ushirikiano wa kutosha wanakamati watakaozunguka kufanya zoezi hilo la uhakiki katika maeneo yao bila kusababisha uvunjifu wowote wa amani.

“Niwambieni ndugu wananchi ninataka nikiamka Januari Mosi mwakani kila mtu awe kwenye eneo lake akifanya shughuli zake bila hofu yoyote, tukifanya hivyo tutaweka historia ya kuwa wilaya ya kwanza kumaliza migogoro ya ardhi kwa njia ya kistaarabu zaidi na wengine wataiga kwetu,” amesema Makonda.

No comments

Powered by Blogger.