Hivi Ndivyo Helikopta Ilivyomuua Shujaa Deo Filikunjombe...Mashuhuda Waelezea Kilichotokea
Polisi na wananchi wakiwa eneo la tukio baada ya Chopa kuteketea kwa moto.
AJALI ya chopa
(helikopta) iliyotokea usiku wa kuamkia jana, Oktoba 16, 2015 katika
Hifadhi ya Selous, eneo la Msolwa mkoani Morogoro, imeyakatisha maisha
ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo la ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe (43),
pamoja na watu wengine watatu waliokuwa ndani ya helikopta hiyo.
Deo Filikunjombe.
Kwa mujibu wa
taarifa zilizothibitishwa na Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi
la Polisi, Paul Chagonja, Mhe. Filikunjombe aliyekuwa akitetea ubunge wa
jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa na watu
wengine watatu kwenye helikopta hiyo, akiwemo rubani, Kepteni William
Silaa ambaye ni baba wa Jerry Silaa, Vitalis Blanka Haule anayetajwa
kuwa ndugu wa Filikunjombe na Egdi Mkwera, Ofisa Tawala wa Mkoa wa
Tarime na mtaalam wa mifugo.
Chopa (helikopta) aliyokuwa akitumia Mbunge wa jimbo la ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe (43).
Chagonja
alieleza kuwa helikopta hiyo yenye namba za usajili, 5Y-DKK ilikuwa
ikitokea jijini Dar es Salaam kuelekea kusini huku taarifa nyingine
zikieleza kuwa ilikuwa ikielekea jimboni kwake, Ludewa kabla ya kupata
hitilafu ya injini ikiwa angani, baadaye ikaanguka na kulipuka,
ikisababisha eneo lote la ajali kugubikwa na vumbi na moshi mzito.
Deo Filikunjombe akiwa kwenye helkopta anayodaiwa kupata nayo ajali.
Habari zisizo
rasmi zilizolifikia gazeti hili, zilieleza kuwa helikopta hiyo iliondoka
jijini Dar es Salaam majira ya saa 9 alasiri. Kabla ya kuruka angani,
vyanzo vyetu vinaeleza kuwa helikopta hiyo ilipata hitilafu ndogo za
kiufundi ambazo hata hivyo zilirekebishwa na safari ikaanza bila
matatizo.
“Ilipofika
kwenye Hifadhi ya Selous, rubani aligundua kwamba kuna hitilafu kwenye
injini, akawa anajaribu kutafuta sehemu ya kutua kwa dharura ndani ya
hifadhi hiyo lakini kabla hilo halijatimia, helikopta ilipoteza mwelekeo
kabla ya kudondoka na hatimaye kulipuka,” kilieleza chanzo chetu kwa
sharti la kutotajwa jina gazetini.
...Wakiendelea kufanya uchunguzi eneo la tukio.
Habari
nyingine zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zinaeleza kuwa
helikopta hiyo ilianza kuwaka moto ikiwa angani kabla ya kuanguka
kandokando ya Mto Ruaha unaopita ndani ya hifadhi hiyo ambapo baadhi ya
maoni yalidai huwenda chopa hiyo ilihujumiwa na hivyo kutaka uchunguzi
zaidi.
Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu usiku wa kuamkia jana, aliandika
kuhusu ajali hiyo kupitia mitandao ya kijamii ambapo alieleza kupata
taarifa kutoka kwa askari wa wanyamapori ndani ya hifadhi hiyo kubwa
kuliko zote nchini Tanzania na kueleza hatua zilizochukuliwa:
“Mashuhuda wa
ajali ya helikopta iliyotokea Selous walikuwa kitalu R2 na walishuhudia
ikianguka na kulipuka ng’ambo ya Mto Ruaha Kitalu R3, maafisa na askari
wanaelekea eneo la tukio kutokea Msolwa na Matambwe na tumeagiza vikosi
vilivyo kwenye doria Selous kushiriki uokoaji.”
Habari zaidi
kutoka vyanzo vyetu, zinaeleza kuwa kutokanana jografia ya eneo ajali
hiyo ilipotokea, iliwachukua muda mrefu maafisa usalama na askari kufika
eneo hilo, kutokana na ugumu waliokutana nao kuvuka Mto Ruaha hasa
wakati huo wa usiku. Hata hivyo, askari na maafisa hao waliendelea
kuhangaika usiku kucha mpaka siku iliyofuatia (jana Ijumaa),
walipofanikiwa kufika eneo la tukio lakini tayari walikuwa wamechelewa
kwani Mhe. Filikunjombe, Kepteni Silaa na wenzao wawili, tayari
walishakata roho.
Naye Jerry
Silaa, Meya wa Manispaa ya Ilala ambaye pia ni mtoto wa rubani wa
helikopta hiyo, jana mchana aliandika kupitia ukurasa wake wa Instagram:
“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa timu ya
uokoaji iliyofanikiwa kufika eneo la ajali na kukuta abiria wote na
rubani wamepoteza maisha.
Kifo cha
Filikunjombe, kimetokea siku 9 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania na
muda mfupi baada ya vifo vya wanasiasa wengine wawili, aliyekuwa Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda na Dk. Emanuel Makaidi,
aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha NLD na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Baadhi ya
wananchi wa gazeti hili waliopata nafasi ya kutoa maoni yao kufuatia
mfululizo huo wa vifo vya viongozi wa kisiasa, walionesha wasiwasi
mkubwa na kuhoji kinachoendelea nchini huku wengine wakihisi ni mambo ya
kafara.
Enzi za uhai
wake, ukiachilia mbali ubunge, Mhe. Deo Filikunjombe alipata kuwa Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyosimamia
kidete sakata la ufisadi wa Escrow na kusababisha viongozi kadhaa
wakubwa serikalini kung’oka kwenye nyadhifa zao. Mungu azilaze roho za
marehemu wote mahalipema peponi, Amen!
Source:GPL
Source:GPL
No comments