Mtuhumiwa wa mauaji ya kinyama mkoani Arusha afikishwa mahakamani
Mtuhumiwa wa mauaji katika Hoteli ya A Square Belmont jijini Arusha, Elijus Lyatuu , ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tano wa masomo ya falsafa katika Chuo cha Kanisa la Katoliki Segerea jijini Dar es Salaam, amepandishwa kizimbani na kusomewa shtaka la mauaji.
Mtuhumiwa huyo, alifikishwa mahakamani jana saa 4:30 asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili PT 1434.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Lilian Mmasi, alidai mbele ya Hakimu Nestory Barowa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kwamba mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa la kumuua Alfred Kimbaa maarufu kwa jina la Mandela (18), Agosti 30, mwaka huu ndani ya Hoteli ya Belmont jijini hapa.
Alidai mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Hata hivyo, aliomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutaja kesi hiyo kutokana na madai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Kwa upande wake, hakimu Baro alimweleza mtuhumiwa huyo kuwa kesi inayomkabili haina dhamana, hivyo atalazimika kuendelea kukaa mahabusu hadi shauri hilo litakapoanza kusikilizwa.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 23, mwaka huu itakapokwenda kwa ajili ya kutajwa tena.
No comments