Header Ads

Gaidi wa Kisomali auawa na kuzikwa kwa siri kwenye Msitu wa Mkuranga


MTU ambaye ametajwa kuwa ni gaidi mwenye asili ya Kisomali (jina lake halikupatikana) ambaye imeelezwa alijeruhiwa kwa risasi katika mapambano kati ya magaidi na
askari wa Kituo cha Polisi Stakishari, Dar Julai 12, mwaka huu, amefariki dunia na kuzikwa kwa siri, Uwazi liko kazini.

Baada ya kifo hicho, inadaiwa magaidi wenzake waliuzika mwili wake kwenye kaburi hilo lililopo kwenye msitu wa Kijiji cha Mamndikongo, Mkuranga, Pwani bila wanakijiji kujua.

UWAZI LIMECHIMBA HIVI
Taarifa zilizopatikana toka vyanzo vyetu makini katika kijiji hicho zinadai kwamba, kaburi la gaidi huyo liligundulika Jumatatu iliyopita. Na hatua chache mbele zikapatikana bunduki mbili aina ya SMG sanjari na risasi kadhaa kufuatia msako mkali ulioendeshwa na wanakijiji kwa ushirikiano wa polisi.

Askari na wananchi eneo la tuikoMara baada ya taarifa hizo, Uwazi lilifunga safari hadi kijijini hapo kwa lengo la kuujua ukweli ambapo Mtendaji wa Kijiji cha Mamndikongo, Issa Said Mchalaganga alikuwa na haya ya kusema:
“Ni kweli kuna msako mkali unaoendeshwa na askari polisi, vyombo vya usalama kwa ujumla na wananchi wa kijiji hiki ambapo Jumatatu iliyopita tulifukua sehemu tuliyoitilia shaka na kukuta mwili wa mtu mwenye asili ya Kisomali.”

HALI YA MAITI
“Maiti tuliikuta imevaa t-shirt yenye alama ya pundamilia, jaketi lenye maandishi ya King Lion (mfalme simba), bukta, pensi, trak’suti ya kuteleza na raba na ilionesha ni mtu mwenye asili ya Somalia kutokana na nywele na sura. Pia alikuwa na madevu.
“Alikuwa pande la mtu, mwenye kifua kipana. Tulipomwangalia vizuri alionekana kuwa na urefu wa kama futi 5.8 na umri tulioukadiria kuwa ni kati ya miaka 45 hadi 50.”

KISA CHA MSAKO
“Tulianza msako mkali katika maeneo ya mashamba ya watuhumiwa hao ambao baadhi yao wamekamatwa na wengine kukimbia nyumba zao baada ya kugundua kuwa, wanasakwa na polisi. Hii ni kufuatia kurejea kwao kijijini hapa nyakati za usiku wa saa tatu kwa siku tatu kabla ya maiti hii kupatikana.
“Taarifa tulizozipata ni kuwa, siku hiyo walifika usiku na pikipiki zaidi ya sita na kuziegesha sehemu iliyokuwa makazi yao kwa lengo la kwenda kwenye maskani yao ya zamani. Lakini walipofika karibu na nyumba ya mtu anayeitwa Joseph Chacha, mbwa wa hapo alibweka wale magaidi wakampiga risasi na kufa. Waliposonga mbele walimuona mbuzi akipita, wakafikiri ni mbwa, naye wakampiga risasi, akafa.”

WAKUTA MAZINGIRA TATA
“Taarifa tulizozipata ni kwamba waliposonga mbele walikuta mazingira ya sehemu waliyokuwa wakiishi yamebadilika. Kulifyekwa hali ilyowafanya wapatwe na hofu na kuamua kuondoka.
“Baada ya taarifa hizo, ndipo sisi tuliwasiliana na polisi na kwenda kuangalia kilichowaleta. Sasa katika msako wa kutafuta tukaona hilo kaburi.”

BENDEJI YAZUA MASWALI
Mtendaji huyo alizidi kusimulia: “Pia tulifukua dawa na bendeji ambayo ilikuwa na masalia ya damu hali iliyoashiria kwamba, alikuwa akitibiwa majeraha ya risasi akashindwa kupata nafuu kwani. Sehemu za mwili wake hasa zile zilizoingia risasi ziliharibika sana.

Silaha zilizokutwa karibu na kaburi la gaidi huyoMAGAIDI WANA DAKTARI WAO
“Daktari alikuja akaufanyia uchunguzi mwili kisha akaruhusu uzikwe tena. Lakini pia kwa upande wao, inasemekana watu hao pia wana daktari wao ambaye alikuwa akiwatibu pale wanapojeruhiwa wakati wa mapambano, sasa na yeye ametoweka.”
KWA NINI MAGAIDI BADO WANARUDI KIJIJINI?
“Watu hao wanaonekena kutafuta namna ya kurudi hapa kijijini kwa sababu kuna vitu vyao, zikiwemo silaha walizoficha ardhini sehemu mbalimbali ila wanashindwa kuja moja kwa moja.”
WANAKIJIJI WASHINDA KWA HOFU
Naye Mkufunzi wa Mgambo Kata ya Bupu na Kamanda wa Kijiji cha Mamndikongo, MG 357062 Abdallah Twalib Mandale alisema kwa sasa wananchi wa kijiji hicho wana hofu kiasi kwamba wanashindwa kuendelea na shughuli zao ili kushiriki katika msako wa silaha za magaidi hao.
WANAKIKIJI WAPONGEZA
Hata hivyo, wanakijiji hao walimpongeza Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na vyombo vyote vya ulinzi na usalama ambavyo vimekuwa vikiendesha oparesheni hiyo ambayo imeleta mafanikio makubwa pia wameiomba serikali kuwapatia vyakula na maji askari wanaojihusisha na zoezi hilo kwani wamekuwa wakifanya kazi porini kwa muda mrefu bila kula wala kunywa maji jambo ambalo ni hatari.

No comments

Powered by Blogger.