Header Ads

Mke wa Dk Slaa akana kumfungia mumewe chumbani

Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuzungumza na kusema yupo salama, mke wake, Josephine Mushumbusi amekanusha tuhuma zilizozagaa kuwa ndiye aliyemshauri kiongozi huyo wa Chadema kujiuzulu na kumzuia kushiriki vikao muhimu vya chama.

Tetesi hizo zilivuma kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari baada ya Dk Slaa kutoonekana katika vikao muhimu vya Chadema na Ukawa, kuwa Mushumbusi hakupendezwa na kitendo cha Lowassa kupitishwa kuwania urais chini ya mwavuli wa Ukawa na badala yake alitaka Dk Slaa ndiye awe mpeperusha bendera.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo Mushumbusi amezikanusha, aliamua kumfungia ndani Dk Slaa kama moja ya mbinu za kumzuia asishiriki shughuli za kichama, tuhuma ambazo amezikanusha.
“Bosi wako akija kukuomba ushauri utamsaidia, lakini akija akakuambia ameshafanya maamuzi unaweza kupingana naye?” alihoji Mushumbusi akianza kutoa maelezo yake na kuendelea:

“Wakati wa vikao nilikuwa namwona (Dk Slaa) anachelewa kurudi kila siku, siku moja akaja akaniambia uamuzi aliouchukua na mimi sikuwa na la kusema, nikachukua shuka nikajifunika.”

Katika mahojiano yake ya kwanza  baada ya kuzagaa kwa tetesi hizo, Mushumbusi pia alikana kumfungia Dk Slaa ndani ya nyumba, akisema wakati maneno hayo yalipokuwa yanazagaa, alikuwa nje ya nchi na wala hakujua kinachoendelea.

“Mwenyewe najiuliza nini kinaendelea, siwezi kufanya kitu kama hicho. Nyumba yangu ina milango miwili, nawezaje kumfungia mtu, tena mwanamume, hata watoto siwezi kuwafungia. Kuna mambo mengine mwanamke huwezi kuyafanya kwa mwanamume. Mwanamume ni mwanamume tu,” alisema.


Alisema viongozi wa Chadema, ndugu, jamaa na marafiki walikuwa wanafika nyumbani kwake na walikutana na Dk Slaa na kuzungumza naye... “Kama ningekuwa nimemfungia wangezungumza naye vipi?”

Mushumbusi alisema mwanamke anaweza kufanya chochote lakini kuna baadhi ya mambo ambayo mwanamume akiamua ni vigumu kumzuia.

Akifafanua tuhuma za kumshinikiza Dk Slaa kujiuzulu Chadema, Mushumbusi alisema kiongozi huyo wa Chadema ana uamuzi wake na yeye ni msaidizi tu ambaye hana uamuzi wa mwisho kwenye familia.

Hata hivyo, alisema endapo angeamua kumshawishi, uwezo wa kufanya hivyo anao lakini yeye ni mwanamke mwadilifu anayependa mafanikio ya mumewe.

“Kwani unanionaje? Mimi ni ‘strong’ (nina nguvu), ningetaka ningefanya hivyo, nisingeshindwa,” alisema.

Pamoja na hayo, Mushumbusi alilalamika kuwa tuhuma hizo dhidi yake zimesababisha asisikilizwe kama ilivyokuwa awali.


Bila kufafanua kwa undani, alisema kuna kundi linalounda propaganda hizo ili abadili mtazamo kuhusu mumewe lakini jambo hilo haliwezi kutokea.

“Nilisema nitampenda kama alivyo, sitajali chochote wala akiwa katika hali gani au chama gani. Kazi yangu ni kumtia moyo ili kile atakachofanya kifanikiwe,” alisema.

Mbali na kukanusha vikali tuhuma hizo, Mushumbusi alisema alikwishajitoa kwenye masuala ya siasa kwa miaka miwili sasa na badala yake ameamua kufanya biashara ya kuuza mkaa.

“Nimenyamaza kimya, nimekaa kando ninaendelea na biashara yangu ya kuuza mkaa, nipo mbali na siasa na sitaki kujua kinachoendelea, kwanza hata mchakato wenyewe siujui,” alisema.

Aliwashauri wanawake kuacha kushabikia masuala yanayotokea ndani ya ndoa yake na kuwataka wavae viatu anavyovivaa na wajue kuwa anapitia wakati mgumu.

No comments

Powered by Blogger.