Header Ads

Mwanamke apandishwa kizimbani baada ya kushindwa kulipia chumba alichokitumia Hotelini siku ya Valentine,......

Mwanamke wa miaka 27 alishtakiwa Jumatano katika mahakama ya Nairobi kwa kushindwa kulipa bili ya hoteli ya kifahari kwa huduma alizopata kwa muda wa siku 21 ikiwemo siku ya wapendanao almaarufu Valentine. Laura Oyier Ogolla, ambaye ni mwanamuziki, alikabiliwa na shtaka la kushindwa kulipa hoteli ya Inter-Continental kitita cha Sh229,505.
Laura alionekana mtulivu akiwa mbele ya Hakimu Mkazi Edda Agade katika Mahakama ya Milimani aliposomewa shtaka. Ogolla, aliyekuwa amejipodoa na kuvalia nadhifu, alikanusha shtaka la kutolipa hoteli hiyo ya kitalii.

Mashtaka yalisema kuwa alipokea huduma mbalimbali katika hoteli hiyo ya kimataifa huku akijifanya alikuwa na uwezo wa kugharamia huduma alizopokea. Upande wa mashtaka unaoongozwa na Inspekta Mkuu Alice Njeru unadai kuwa mshtakiwa alikuwa akijificha na kurudi hotelini usiku wa manane na kuingia chumbani mwake bila ya kuonekana na maafisa wa mapokezi wa hoteli hiyo.

Lakini ujanja wake uligonga mwamba alipotembelewa na afisa mmoja wa ngazi ya juu chumbani mwake. Alichunguzwa na mnamo Februari 16 akatiwa nguvuni na maafisa wa polisi. Alizuiliwa katika kituo cha Polisi cha Central kutoka Februari 16 hadi Jumatano alipofikishwa kortini.

Mshtakiwa aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana, ombi ambalo halikupingwa na upande wa mashtaka.

Hakimu Agade alimwamuru Ogolla alipe dhamana ya pesa taslimu ya Sh100,000 na kuorodhesha kesi  dhidi yake isikizwe Aprili 15.

Pia aliamuru upande wa mashtaka umkabidhi mshtakiwa nakala zote za mashahidi pamoja na stakabadhi nyingine zitakazotegemewa katika kesi hiyo kama ushahidi ndipo aandae tetesi zake.

No comments

Powered by Blogger.