Header Ads

UNYAMA: MTOTO AFUNGIWA NDANI YA BOKSI NA MAMA YAKE MLEZI ILI ASIMWAMBUKIZE VIRUSI VYA UKIMWI

Unyama huo wa kusikitisha, umefanyika muda wote huo kwa mtoto huyo Morogoro mjini katika mtaa wa Azimio bila kuripotiwa popote, huku wakazi na majirani wa nyumba hiyo wakisikia akikohoa na kulia usiku, na baba yake mzazi akiendelea na maisha kwa kumuogopa mkewe.

Wakizungumza na mwandishi jana, majirani hao walidai Mariam alihamia katika nyumba hiyo mwaka 2010, lakini hawakuwahi kumuona akiwa na mtoto.

Hata hivyo majirani hao walikiri kwamba walikuwa wakisikia mtoto akikohoa na kulia hasa nyakati za usiku, lakini walikuwa na wasiwasi kuwa huenda mtuhumiwa alikuwa mshirikina anayefuga watu waliouawa kishirikina au kwa jina lingine misukule.

Mtoto wa miaka minne (jina limehifadhiwa), amedhulumiwa haki yake ya utu na kuteswa kwa zaidi ya miaka mitatu, kwa kufungiwa ndani ya boksi kama mnyama, ili asimuambukize mama mlezi virusi vinavyosababisha Ukimwi. 
Hatimaye juzi mateso ya mtoto huyo yalipungua, baada ya msamaria mmoja kupata taarifa sahihi, kwamba ndani ya nyumba hiyo kuna kiumbe asiye na hatia aliye katika mateso na kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo.

Zongo akiwa katika kazi za kawaida katika mtaa huo, alipata taarifa kutoka kwa majirani kuwa kuna mwanamke, Mariam Said, amemficha mtoto ndani ya boksi na hamfanyii usafi wala kumtoa nje.

Mtoto Nasra akiwa katika wodi ya watoto hospitali ya mkoa wa Morogoro anakopatiwa matibabu kwa sasa

Baada ya kupata taarifa hizo, Zongo alimtafuta mwenyeji wake, Mwenyekiti wa mtaa huo, Tatu Mgagalana na kuongozana naye hadi kwenye nyumba hiyo ambapo walimkuta mtuhumiwa, Mariam na kuanza kumhoji kuhusu tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa Zongo, wakati mtuhumiwa akijibu maswali aliyoulizwa huku akibabaika, ghafla mtoto huyo alipiga chafya na kuanza kukohoa hali iliyowapa wasiwasi na kuamua kuingia chumbani kwa Mariam kwa nguvu, hatua iliyomuokoa mtoto huyo kutoka katika mateso ya zaidi ya miaka mitatu.

Ofisa huyo na mwenyeji wake walimkuta mtoto huyo ametapakaa uchafu uliotokana na kinyesi na mkojo, kwa kuwa boksi hilo lilikuwa chumba chake cha kulala, meza yake ya chakula na maji na choo kwa ajili ya haja ndogo na kubwa.

Hali ya mtoto huyo ilisababisha mashuhuda waliokuwa wamezunguka nyumba hiyo, kuanza kumshambulia Mariam kwa fimbo na mawe, na kumlazimu Zongo na mwenyeji wake kufanya kazi ya ziada kumnusuru mtuhumiwa kwa kutoa taarifa Polisi, huku wakijaribu kuzuia asidhurike.

Baada ya muda askari Polisi walifika na kumchukua mtuhumiwa na alipofika kituoni, inadaiwa alikiri kuanza kumlea mtoto huyo tangu akiwa na miezi tisa baada ya mama yake, kufariki dunia mwaka 2010.

Mtuhumiwa huyo alidai Polisi kuwa kwa mara ya mwisho, alimuogesha mtoto huyo Julai mwaka jana, na alikuwa akimwekea chakula na maji ndani ya boksi hilo.

Mume wa mtuhumiwa huyo, Mtonga Ramadhani ambaye ni mfanyabiashara wa Soko la Mawenzi katika Manispaa ya Morogoro naye alikamatwa na katika mahojiano, alidai hakuona sababu ya kutoa taarifa za kufichwa kwa mtoto huyo kwa sababu hamhusu na wajibu wake ilikuwa kutafuta chakula tu.

Kwa sasa mtuhumiwa huyo yupo Kituo Kikuu cha Polisi mjini Morogoro na mtoto amepelekwa katika Ofisi ya Idara ya Ustawi wa Jamii.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, alidai baada ya mzazi mwenzake kufariki dunia, alishindwa kumchukua mtoto wake kwa sababu tayari alishakuwa na mke.

Alidai kwa kuwa alikuwa ameoa, alikubaliana na upande wa pili wa familia ya marehemu, kuwa mwanawe huyo alelewe na mama yake mkubwa, Mariam.

Akizungumzia ulemavu wa mtoto huyo, Ofisa Ustawi wa Jamii, Oswin Ngungamtitu alisema ulemavu huo huenda umetokana na kuishi kwenye boksi tangu akiwa na miezi tisa hadi sasa bila kutolewa nje, kufanyiwa usafi wala kupewa chanjo mbalimbali ikiwemo ya polio.

Ngungamtitu alisema ulemavu huo pia huenda umetokana na kukosa lishe yakiwemo maziwa ya mama, hewa safi na upendo na kwamba mtoto huyo atakuwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo minyoo, nimonia, utapiamlo na malaria.

Kutokana na hali hiyo, Ngungamtitu alisema ofisi yake imempeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ili akafanyiwe uchunguzi na kupewa chanjo ya kutibu magonjwa yatakayobainika.

Baada ya hapo kwa mujibu wa Ofisa huyo, mtoto huyo atapelekwa kwenye kituo cha kulelea watoto yatima na ikibidi atakabidhiwa kwa baba yake mzazi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, mwanamke huyo pamoja na mumewe wanashikiliwa Polisi kwa kosa la kumfanyia ukatili mtoto kinyume cha Sheria ya Mtoto ya 2009


SOMA ZAIDI HAPA TUKIO HILO:

Mkazi wa Mtaa wa Azimio, Kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, Mariam Said ( kati kati) akizindikizwa kwenda Kituo Kikuu cha Polisi na Askari Polisi wa kike ,juzi ( Mei 20) baada ya kutoa maelezo kwa Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu ( hayupo pichani) kutokana na madai ya kufanya vitendo vya ufanyasaji na ukatili mtoto wa mdogo wake baada ya kufariki dunia, kwa kulea mtoto, huyo wa kike mwenye umri wa miaka ninne ambapo yenye na mumewe , Mtonga Omary ,( hayupo pichani) walipoamua kumfungia chumbani na kwenye boski kwa muda miaka yote hiyo.
Mkazi wa Mtaa wa Azimio, Kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, Mtonga Omary ( kati kati) akizindikizwa kwenda Kikuu cha Polisi na Askari Polisi wa kike baada ya kutoa maelezo kwa Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu ( hayupo pichani) kutokana na madai ya kufanya vitendo vya ufanyasaji na ukatili yeye na mkewe Mariam Said ( hayupo pichani) kwa kumfungia chumbani na kwenye bokis mtoto wao wa kike wa kumlea mwenye umri wa miaka minne.
Askari Polisi wa Kike ( kushoto) ambaye jina lake hakikuweza kufahamika mara moja akimwesha juisi ,mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne ( jina linahifadhiwa) aliyekuwa amefungiwa ndani ya chumba kwa kipindi cha muda wa miaka minne na kukaa ndani ya boksi kwenye nyumba iliyopo Mtaa wa Azimio, Kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, ( wapili kushoto) ni mama mlezi Mariam Said ( kati kati),ni baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi na ( kulia) ni baba mlezi wa mtoto , Mtonga Omary, hapawalikuwa wakitoa maelezo mbele ya Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu ( hayupo pichani).

No comments

Powered by Blogger.