Header Ads

Taadhari picha zinatisha......Mama mzazi amchoma mwanaye moto....

Dunia haina huruma! Mtoto Samwel Paulo (13), anayesoma darasa la nne Shule ya Msingi Amani wilayani Ilala, Dar, amelazwa wodi ya watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akiendelea kuuguza majeraha yaliyotokana na kile kinachodaiwa ni kulipuliwa kwa moto na mama yake mzazi aliyetajwa kwa jina la Doricus Iganga.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea nyumbani kwao maeneo ya Mombasa Gongo la Mboto, Dar mwishoni mwa wiki iliyopita, saa 8:00 usiku ambapo mwandishi wa habari hii alimtembelea wodini hapo.

Alipoulizwa kisa na mkasa hadi kuwa katika hali mbaya kiasi hicho, mtoto huyo alikuwa na haya ya kusema: “Najisikia vibaya sana kutokana na maumivu makali ya moto. Sikutegemea kama mama yangu mzazi angenifanyia hivi kwa kunituhumu kuwa nimemuibia fedha zake shilingi elfu kumi.
“Amekatisha ndoto yangu ya masomo, kwa sasa wenzangu wanajiandaa na mtihani wa muhula, mimi nipo wodini.
Mtoto Samwel Paulo akiwa hospital baada ya kufanyiwa kitendo cha kinyama na mama yake mzazi.


“Matukio kama haya huwa nimekuwa nikiyasikia yakifanywa kwa watoto wenzangu kutoka kwa mama wa kambo na siyo kwa mama mzazi kama ilivyotokea kwangu.

“Kwa hali hii hakuna mtu anayeweza kunionea huruma kama mzazi wangu hana uchungu na mimi. Sitegemei kuendelea kuishi na mama endapo Mungu akinisaidia nikapona. Ninachokikumbuka ni kwamba siku hiyo nilitoka shule, ilipofika saa 12:00 jioni, mama akawa amerudi kutoka katika kibarua chake.
Mtoto Samwel Paulo akiwa na maumivu makali hospitalini.


“Alitupatia fedha ya kununua chipsi kwa sababu alikuwa anaondoka kwenda kwenye shughuli yake nyingine ya kuuza chakula maeneo ya Ukonga-Mazizini.

“Aliporudi usiku, mimi na mdogo wangu Salim Paulo (10), tulikuwa tumeshalala. Nakumbuka ilikuwa saa 8:00 usiku, mama alituamsha akawa anasema mimi na mdogo wangu tumemuibia fedha hasa mimi.

“Nilimkatalia kwamba sijachukua wala sikujua alipoiweka, hakunisikiliza, alichukua mafuta ya taa na kunimwagia kisha akanilipua na kutokomea kusikojulikana.
“Mdogo wangu alichukua maji kwenye ndoo na kunimwagia hadi moto ukazimika.
“Niliungua vibaya sana. Baada ya muda mfupi alirudi akijifanya yeye hahusiki, niliishiwa nguvu, nilipoteza fahamu.

“Nilikuja kujitambua nikiwa hospitalini Amana. Hali ilikuwa mbaya ndipo nikaletwa hapa Muhimbili na ninauguzwa na bibi yangu baada ya mama kukamatwa na polisi.
“Nawashukuru sana madaktari na wauguzi kwa kunihudumia kwa karibu.

Naona mabadiliko kidogo ingawa tumbo linaniuma kwa ndani,” alisema mtoto huyo kwa masikitiko makubwa.

Kwa upande wake, bibi yake, Helen Barnaba anayemuuguza mtoto huyo baada ya mama yake kukamatwa na polisi alikuwa na haya ya kusema:

“Nikiwa kwangu Igunga, Tabora, nilipigiwa simu kuwa mjukuu wangu kaunguzwa moto, nilizimia, nilipozinduka nikaanza maandalizi ya kuja Dar.

“Nilipofika na kukuta hali kama hii, sikuamini kama mwanangu angeweza kufanya jambo kama hili.
“Hata hivyo, hii siyo bure bali ni mzunguko wa shetani, hawa wajukuu nilikuwa nikiishi nao kwa muda mrefu hadi pale nilipougua, nikamwambia mama yao awachukue.”

Mtoto huyo kwa sasa yupo hospitalini akiendelea na matibabu huku mama yake mzazi akishikiliwa kwenye Kituo cha Polisi cha Sitaki-Shari, Dar kwa upelelezi ili sheria ichukue mkondo wake.

Kwa yeyote atakayeguswa na kisa cha mtoto Samwel, anaweza kufika katika wodi hiyo ya watoto au kuwasiliana na bibi yake anayemuuguza kwa namba 0762 389774. Pia anaweza kumpatia msaada wa fedha kwa namba hiyo, tunamuombea mtoto huyo apone ili akajiunge na wanafunzi wenzake katika masomo.

No comments

Powered by Blogger.