Header Ads

WANAUME HUPENDA KUOA MWANAMKE WA AINA HII

Habari za wiki hii mpenzi msomaji. Mimi namshukuru Mungu kwa kuweza kunikutanisha na nyinyi kupitia safu hii ambayo pamoja na mambo mengine nazungumzia juu ya mada mbalimbali ambazo zinagusa maisha yetu ya kila siku.

Wiki hii nitazungumazia juu ya aina ya wanawake ambao wanaume wengi hupendelea kuoa. Wanaume wengi wanapofikia hatua ya kuoa si kwamba wanakurupuka tu na kuoa mwanamke yeyote mwenye sura nzuri, bali huchukua muda wao mwingi kuchunguza mambo mengi juu ya wake ambao wanadhani kwamba wanaweza kuwa pamoja kwa kipindi chote cha maisha.
Wanawake wengi wanajisahau na kudhani kwamba kitu kinachoweza kuwafanya wakapata wachumba ni uzuri hivyo kupoteza muda wao kujichubua na kujiremba ili wawavutie wanaume bila kujua kwamba kuolewa ni zaidi ya uzuri.
Hali sasa hivi imebadilika ni tofauti na kipindi cha nyuma ambapo ukiwa na sura nzuri na umbo la kuvutia basi una asilimia 100 za kuolewa. Utafiti ambao nimeufanya unaonesha kwamba zaidi ya uzuri wa tabia na umbo, kuna kuna sifa nyingine za msingi ambazo mwanamke anatakiwa kuwa nazo ili aweze kuwa katika mazingira mazuri ya kupata mchumba wa kumuoa kiasi kwamba asipokuwa nazo ataishia kuchezewa tu lakini haitatokea mtu kumtakiwa kwamba anataka kumuoa.

MWEYE MAPENZI YA KWELI
Lengo kubwa la mwanaume kuoa ni kutaka kupata mapenzi ya kweli kutoka kwa mwanamke na ikiwezekana waweze kupata watotoa ambapo watoto mara ndio wamekuwa furaha ya ndoa. Wapo wanawake wengine ambao wanonesha wazi kutokuwa na mapenzi ya kweli bali wanakuwa na mapenzi ya kuzuga. Wanachotaka wao aidha kupata umaarufu tu kwamba yuko na mtu fulani ama kuweza kupata pesa alizonazo mwanaume lakini sio kwamba ana mapenzi ya dhati kutoka moyoni mwake. Mwanamke asiye na mapenzi ya dhati utamgundua tu, muda mwingi utamuona macho yake yako kwenye mfuko wa mwanaume. Akiona kwamba mfuko umetuna utaona anaonesha mapenzi ya hali ya juu lakini pindi hali inapokuwa kubwa mbaya kifedha mapenzi yanaanza kufifia.
Kwanini wanaume wanapenda wana wake wenye mapenzi ya dhati kutoka mioyoni mwao na si kutokana na fedha walizonazo? Hii inatokana na ukweli kwamba maisha  siku zote yanabadilika, kama waswahili wanavyosema, kuna kupanda na kushuka.Sio kwamba kila siku utakuwa na maisha mazuri na kama itatokea hivyo basi ushukuru mungu.Hivyo basi mwanamke wa kuoa lazima afahamu hivyo na awe tayari kuonesha mapenzi yake ya dhati wakati wote wa maisha yao na si kwa kipindi fulani tu cha neema.

Si hivyo tu pia asilimia kubwa ya  maisha ya  ndoa yanatawaliwa na mapenzi, kwa hiyo nyanja hiyo inakuwa ya msingi sana kwa wanaume wengi kuiangalia  ili wasije wakajikuta wanaoa mwanamke ambaye baada ya muda mapenzi yanakwenda likizo hali ambayo inaweza kuwafanya wasiishi maisha ya raha mustarehe.

WENYE TABIA NZURI
Tabia njema ndio silaha ya maisha, ukiwa na tabia nzuri kila mtu atakupenda, hiyo ni katika maisha ya kawaida. Lakini linapokuja suala na kuoa tabia inakuwa kitu cha awali sana kungaliwa na hiyo inaweza kuwa na ukweli kwa sababu wapo wasichana wazuri wenye mvuto wa aina yake na maumbile mazuri, lakini  wanakosa wanaume wa kuwaoa, ukiuliza kwani utaambiwa  anatabia mbaya. Naweza kusema hilo ndilo limekuwa tatizo kubwa kwa baadhi ya  wanawake kukosa wanaume wa kuwaona. Hakuna mwanaume hata mmoja kati ya wale ambao nimejaribu kuongea naye ambaye ameonesha kulidharau suala hilo la tabia.
Si hivyo tu wapo wanaume  ambao wameingia kichwa kichwa na kuoa kwa kuangalia sura tu bila kujali tabia, matokeo yake baada ya siku chache yanatokea machafuko ya aina yake hali ambayo imepelekea kuvunjika kwa ndoa kutokana na tabia mbaya alizonazo mwanamke.

WENYE UCHU NA MAENDELEO
Hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko ya aina yake kwa wanaume, wengi sasa hivi hawapendi kabisa kuoa mwanamke ambaye hana kazi yaani 'golikipa'. Kama atakuwa hana kazi basi awe na uchu wa maendeleo kwa kujituma kufanya kazi mbalimbali za kimaendeleo kama vile kilimo kwa wale walio vijijini na biashara ndogondogo kwa wale ambao wako mijijini na hata vijijini. Ile dhana ya kusema mwanamke ni mama wa nyumbani wa kukaa na kujipodoa akimsubiria mwnaume arudi amstarehesha, sasa hivi imepitwa na wakati. Wanaume wengi wanapenda wanawake ambao ni wahangaikaji, wenye ndoto za maendeleo katika maisha yao. Hata kama watakuwa si wafanyakazi lakini wawe wenye kutoa ushauri kwa waume zao juu ya jinsi gani wafanye ili wafanikiwe.

WASIOPENDA MAKUU
Kuna  wanawake wengine wanakuwa na tabia za ajabu sana kiasi kwamba yaweza kuwa kero kwa wanaume. Wapo wanawake ambao wanapenda makuu bila kujali hali halisi ilivyo. Kuna wanawake naweza kusema wana tamaa, kila wikiendi utamsikia "leo tunakwenda wapi dear?"  Akimuona rafiki yake kanunua simu ya laki tatu na yeye utamsikia akisema, ‘na mimi naomba uninunulie simu kama  ya Grace’. Ukienda naye Pub anakuambia, "mimi sinywi pombe za chupa natumia za kopo tena Heineken’. Yeye hajali kiasi cha pesa mwanaume alicho  nacho na usipotekelezea anachukia na anaweza hata kupunguza mapenzi.

 Wanawake kama hawa wako katika mazingira magumu sana ya kuweza kupata wanaume wa  kuwaoa.  Mara nyingi katika maisha fedha huzungumza, kama mwanaume atakuwa na pesa ya kutosha itakuwa rahisi sana kwa mwanamke kupata kila atakachopenda lakini si kwa kumwambia mimi nataka kitu fulani.Mwanaune mwenyewe utamsikia akisema, ‘unataka nikununulie simu ya aina gani, au leo unataka twende wapi?’ hapo ndipo utakuwa na nafasi ya kusema, ‘mimi nataka uninunulie simu kama ya fulani ama leo nataka twende sehemu fulani.’
Wanaume ni warahisi sana wa kuwapatia wale ambao wanatarajia kuwaoa chochote ambacho watahitaji kama tu pesa haitakuwa  tatizo. Kitu ambacho kinawaudhi wanaume wengi  ni ile tabia ya mwanamke kupenda mambo makubwa bila kuangalia uwezo uliopo kwa mwanume.
Kuna wanawake wengine wao si wasemaji kabisa, yeye anasubiri leo amemletea hiki, anapokea na kushukuru, kesho akiambiwa twende beach anakubali. Au wengine wanasubiri mpaka waulizwe wanataka nini, ndio wanasema.
Sisemi kwamba uwe mkimya tu hata kama una shida ya kitu fulani na unafahamu kwamba ukimweleza mwenza wako anaweza kukusaidia, hapana! kama unaona kwamba uwezekano wa kupata kile ambacho unakihitaji upo mweleze kwa utaratibu naamini atakuelewa na kukutimizia.Tabia ambayo hawaipendi wanaume wengi ni ile ya kulazimisha ufanyiwe kitu fulani wakati inawezekana uwezekano haupo.

WAVUMILIVU
Wapo wanawake ambao sio wavumilivu kabisa katika maisha.Tunajua kwamba maisha siku zote hayatabiriki, yanaweza kutokea matatizo ya kiafya ama kifedha.Huu ndio wakati wa kuona uvumilivu wa mtu.Kama mwanamke anatarajia kwamba siku zote ni za raha tu na pindi matatizo yanapotokea anachukua uamuzi wa kumtoroka mwanume, huyo siyo mwanamke wa kuoa.Wangapi leo hii huwatoroka waume zao pindi inapotea kuumwa, kufilisika ama kupatwa na tatizo lolote ambalo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kuwafanya maisha yao kutingishika?

Uvumilivu kwa mwanamke utakuwepo kama tu atakuwa na mapenzi ya dhati kama nilivyozungumza hapo awali. Mwanamke mweye mapenzi ya dhati ni lazima atakuwa mvumilivu na atakuwa tayari kuishi katika maisha ya aina yoyote, yawe ya raha ama ya starehe.Hawa ndio wale ambao wanaume wengi wengependa kuwa nao maishani mwao.

Licha ya kupenda kuoa wanawake amabo wana tabia hizo nilizozitaja hapo juu, wanachukizwa sana na wanawake ambao wanavijitabia vidogo vidogo ambavyo kimsingi havikubaliki katka jamii.Tabia hizo ni kama wambea, wasio wakweli na wawazi, wasioridhika, wagumu kusamehe na wapesi wa kuchukia, wagomvi na wenye roho ya kwanini.
 Utafiti huu umefanyikwa kwa baadhi ya wanaume ambao wanatarajia kuoa wanawake ambao wanaoishi katika maeneo mbalimbali jijini Dar-es-Salaam. Kwa maana hiyo basi hiyo iwe changamoto kwa wanawake. Wajue kwamba wanaume wanafurahi kuwa na wanawake wa aina gani. Hata kama utakuwa umeshaolewa, kama kuna wakati kunakuwa na kutokuelewana baina yenu, chunguza yawezekana kwamba unakosa mojawapo ya tabia ambazo nimezitaja hapo juu. Waweza kubadilika kwani inawezekana.
UKIPENDWA PENDEKA ILA USIPENDE SANA NA UWE TAYARI KUUMIZWA!

MAPENZI! Hivi umeshawahi kukaa chini na kujiuliza kwamba, kama yasingekuwepo mapenzi ulimwenguni binadamu wangeishi vipi? Kimsingi ni swali gumu na hakuna anayeweza kulitolea jibu la moja kwa moja. Ni sawa na wanaume wanavyojiuliza kwamba wasingekuwepo wanawake wangeishi vipi.

Ninachotaka kukizungumzia leo ni kwamba, mapenzi yamekuwa yakiwasumbua walio wengi katika maisha yao hadi wengine kufikia hatua ya kujilaumu kwa nini wameingia katika ulingo huo.

Wapo ambao wamepoteza maisha kwa sababu ya mapenzi, wapo waliochanganyikiwa na wengine kuathirika tu kisaikolojia kwa sababu ya mapenzi. Pia wapo walioachishwa kazi kwa sababu ya mapenzi. Kimsingi mapenzi ni kitu hatari sana kama hakitawekewa umakini.
Lakini sasa licha ya mapenzi kuleta matatizo kwa binadamu, bado tunaambiwa kwamba, utakuwa peke yako kwa muda fulani wa maisha yako na mwishowe utatakiwa kutafuta mwenza ambaye utaishi naye kama mume na mke.
Swali la kujiuliza ni kwamba, je kama kila unapoingia katika mapenzi unaumizwa na mtu ambaye umempenda na ungetamani siku moja muoane, kuna ulazima wa kuendelea kung’ang’ania penzi lake? Na kama utaendelea kuling’ang’ania penzi la mtu ambaye anakuumiza kila wakati bila kujali, itakuwa inaleta maana?
Kimsingi katika maisha ya sasa hasa kwa wale ambao bado hawajaolewa au kuoa, wanatakiwa kuwa tayari kupenda na kupendwa lakini pia wanatakiwa kutopenda sana kwani madhara yake ni makubwa. Pia wawe tayari kuumizwa kwanza kabla ya kumpata yule mwenza mweye mapenzi ya dhati kwao.
Mapenzi ya sasa yamejaa usanii wa hali ya juu kiasi kwamba ukifanya uchunguzi utabaini wengi walio katika uhusiano wa kawaida yaani ‘boyfriend & girlfriend’ wanapitisha muda tu lakini uwezekano wa wao kuja kuwa kitu kimoja ni mdogo sana.
Unaweza kuwa katika uhusiano na mtu akawa anakuonesha mapenzi ya kweli mpaka mwenyewe ukajiona mwenye bahati lakini kumbe mwenzako anakufanyia usanii tu. Sasa utajuaje kwamba huyo uliyenaye hana mapenzi ya dhati kwako? Hapo ndipo penye shughuli pevu na ndiyo maana wakati mwingi tunajijengea imani tu. Tunaamini kwamba, kwa sababu ya mambo anayonifanyia mpenzi wangu, ni lazima atakuwa ameniweka moyoni mwake.
Tutambue tu kwamba mapenzi ya kujifanyisha hayawezi kuchukua muda. Utadanganya leo, utadanganya kesho lakini ipo siku mpenzi wako atabaini tu kwamba amedondoka katika penzi lisilo sahihi na hapo ndipo yaweza kuwa mwisho wa penzi hilo la bandia.
Ninachotaka kukushauri wewe msomaji wangu ni kwamba, unapotokea kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu kwa lengo la kutaka kuoana kisha yeye akaja kukuumiza kwa kukufanyia mambo mabaya, chukulia kwamba ni safari ya kuelekea kumpata mwingine mwenye mapenzi ya dhati kwako.
Najua utaumia sana lakini kutakuwa hakuna jinsi, kama yeye kaamua kukuacha huna nafasi ya kulirejesha penzi lake kwako kwa hiyo unatakiwa tu kukubaliana na hali halisi.
Ila sasa baada ya kuumizwa, hutakiwi kukurupuka kutafuta mtu mwingie wa kujaza nafasi hiyo. Hiyo ni mbaya sana kwani unaweza kujikuta unaingia tena katika penzi chungu kuliko hata lililopita. Kaa chini jiulize, mpaka kufikia mpenzi wako kukuacha ni wewe mwenye makosa au ni yeye?
Kama ni wewe lazima ujute kwanza na kuwa tayari kubadilika. Lakini kama utabaini kwamba hukuwa na kosa lolote bali uliyekuwa naye kaamua tu kukuumiza kwa sababu zake anazozijua, hilo muachie Mungu, yeye ndiye atakulipa wewe na aliyekutenda.

No comments

Powered by Blogger.