Header Ads

SIMBA SC SARE 1-1 NA MBEYA CITY

SIMBA SC imegawana pointi na wenyeji Mbeya City baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 Uwanja wa Sokoine Mbeya.
Matokeo hayo yanaifanya Mbeya itimize pointi 35 sawa na Yanga SC iliyo nafasi ya pili kwa wastani mzuri wa mabao wakati Simba inatimiza pointi 32 na inabaki nafasi ya nne.
Hadi mapumziko, tayari Mbeya City walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Deogratius Julius kwa penalti dakika ya 13, akimchambua vizuri kipa Mghana, Yaw Berko.
   Wachezaji wa Mbeya City wakishangilia bao la kuongoza kabla ya Simba 
                            kusawazisha leo Uwanja wa Sokoine


Penalti hiyo ilitolewa kufuatia beki Joseph Owino kuunawa mpira katika harakati za kuokoa krosi ya Deus Kaseke kutoka wingi ya kushoto.
Mbeya City walitawala mchezo na kipindi cha kwanza na Simba SC ilimtumia Ramadhani Singano ‘Messi’ kushambulia, ambaye hata hivyo aliwekewa ulinzi mkali na mabeki wa timu ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Mshambuliaji Mrundi Amisi Tambwe aliunganishia juu ya lango kwa kichwa mipira miwili ya adhabu iliyopigwa na Amri Kiemba kipindi cha kwanza, kufuatia Messi kuangushwa.

Kipa wa Simba SC, Yaw Berko akiwa amepiga magoti baada ya kufungwa kwa penalti leo Uwanja wa Sokoine
Kocha Mkuu wa Simba SC, Mcroatia Zdravko Logarusic kwa pamoja na wasaidizi wake Suleiman Matola na Iddi Pazi waliwafuata marefa katikati ua Uwanja kuwalalamikia walikuwa wanawapendelea wenyeji na kuwaomba kipindi cha pili wachezeshe haki.

Ramadhani Singano 'Messi' wa Simba SC akiwatoka mabeki wa Mbeya City leo

Kipindi cha pili, Simba SC ilibadilika mno na kuongeza kasi ya mashambulizi, hatimaye kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 50 mfungaji Mrundi Amisi Tambwe, aliyemalizia krosi ya Haroun Chanongo.
Baada ya Simba SC kusawazisha, kasi ya mchezo iliongezeka kwa pande zote mbili, timu zote zikishambuliana kwa zamu.

Kikosi cha Mbeya City;
 David Burhan, John Kabanda, Hamad Kibopile/Mwagane Yeya dk31, Deo Julius, Yussuph Abdallah, Anthony Matogolo, Peter Mapunda, Steven Mazanda, Paul Nonga/Francis Castor dk81, Hassan Mwasapili na Deus Kaseke.
Simba SC;
Yaw Berko, William Lucian ‘Gallas’, Henry Joseph, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’/Awadh Juma dk66, Said Ndemla/Christopher Edward dk76 , Amisi Tambwe, Amri Kiemba na Haroun Chanongo/Zahor Pazi dk54.

No comments

Powered by Blogger.