Header Ads

Mtihani wa Kidato cha Nne Kuanza Leo.......NECTA Yatoa Onyo

Watahiniwa 408,442 wamesajiliwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne unaotarajia kuanza leo hadi Novemba 18, mwaka huu.

Akizungumzia maandalizi ya mtihani huo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema kati ya watahiniwa waliosajiliwa wa shule ni 355,995 na wa kujitegemea ni 52,447. Mwaka 2015, waliosajiliwa kufanya mtihani ni 448,382, hivyo kuwapo na upungufu wa watahiniwa 39,940.

Dk Msonde alisema kati ya watahiniwa wa shule 355,447 waliosajiliwa, wavulana ni 173,423 ambao ni asilimia 48.72 na wasichana ni 182,572 sawa na asilimia 51.28. Watahiniwa 59 ni wasioona na wenye uoni hafifu ni 283.

Alisema kati ya watahiniwa wa kujitegemea 52,447 waliosajiliwa, wanaume ni 25,529 sawa na asilimia 48.68 na wanawake ni 26,918 sawa na asilimia 51.32.

Pia watahiniwa wa kujitegemea wasioona wako saba, wanawake watatu na wanaume ni wanne. Mwaka jana watahiniwa wa kujitegemea walikuwa ni 54,317.

Kuhusu watahiniwa waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Maarifa (QT), Dk Msonde alisema baraza limesajili 20,634 ambao wanaume ni 7,819 sawa na asilimia 37.89 na wanawake ni 12,815 sawa na asilimia 62.11. Mwaka jana, idadi ya watahiniwa wa QT walikuwa 19,547.

“Maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na usambazaji wa mtihani, vitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani,” alieleza Dk Msonde.

Aidha, baraza limewaasa wanafunzi, walimu kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wa mtihani kwani watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufutiwa matokeo yote.

Katika matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa wiki iliyopita, wanafunzi 238 kutoka shule sita walifutiwa matokeo yao yote kutokana na udanganyifu wa mtihani.

Dk Msonde alizitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri, kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya Taifa zinazingatiwa ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu. Pia Dk Msonde alitoa mwito kwa wasimamizi wote kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

“Wasimamizi wanaaswa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa Mitihani ya Taifa,” alieleza.
Powered by Blogger.