Header Ads

Hotuba ya Rais Magufuli Baada ya Kuwasili Kenya

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli leo amewasili nchini Kenya kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Baada ya kuwasili katika Ikulu ya Kenya jijini Nairobi, Rais Magufuli amekagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21

Akizungumzia mambo atakayoyafanya, Msemaji wa Rais Kenyatta, Manoah Esipisu, Jumapili aligusia mambo ambayo Kenya inatarajia kutoka kwa ziara ya Rais Magufuli nchini Kenya.

Alisema: “Ziara ya Rais huyu inatupatia fursa ya kufanya upya na kukoleza uhusiano wetu katika nyanja mbalimbali. Viongozi wa nchi hizi watashauriana kuhusu masuala mbalimbali ya pamoja katika ngazi ya taifa kwa taifa na kanda. Wataangazia sana masuala ambayo tayari kumekuwa na mazungumzo, na tunatarajia matokeo ya mazungumzo hayo kutangazwa.

“Masuala kadha yatajadiliwa, ikiwemo ada ya vibali vya kufanyia kazi ambayo raia wa Kenya hutozwa, pamoja na karo ya juu ambayo Wakenya hutozwa vyuo vikuu (Tanzania). Mashauriano kuhusu kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hizi mbili pia yatafanyika. Kadhalika, na muhimu sana katika mazungumzo hayo ni shughuli za magari ya kusafirisha watalii yanayovuka mipaka.

“Muhimu katika mashauriano haya itakuwa pia kufufuliwa kwa Tume ya Ushirikiano wa Pamoja na Tanzania (JCC) ambayo ni jukwaa ambalo linaweza kutumiwa kutangaza biashara na uwekezaji baina ya nchi zote mbili.

“Rais Kenyatta pia atazungumza na Rais Magufuli kumhusu Bi Amina Mohammed (waziri wa mambo ya nje wa Kenya) anayewania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Rais Magufuli akiwa Kenya atatembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen Nairobi na kuzindua barabara mchepuko jijini Nairobi.





Powered by Blogger.