Taarifa Rasmi ya Serikali Kuhusu Tetemeko la Ardhi Mkoani Kagera
1 Tukio la tetemeko:
Tarehe 10/09/2016 saa 9 na dakika 27 mchana kumetokea tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Kitovu cha tetemeko hilo ni kwenye makutano ya latitudo 10 06’ na
longitudo 31055’ eneo ambalo ni kilomita 20 kaskazini mashariki mwa
kijiji cha Nsunga na kilomita 42 kaskazini magharibi mwa mji wa Bukoba
(Picha Namba 1 na 2). Kitovu hicho kilikuwa kilomita 10 chini ya ardhi
kwenye eneo hilo.
Picha Namba 2: Kitovu cha tetemeko la ardhi Kagera (Nyota nyekundu)
Nguvu za mtetemo wa ardhi wa tetemeko hilo ni 5.7 kwa kutumia skeli
ya “Richter” ukubwa ambao ni wa juu sana kiasi cha kuleta madhara
makubwa. Kutokana na ukubwa huu maeneo mengi ya mkoa wa Kagera
ikijumuisha mji wa Bukoba yamepatwa na madhara makubwa sana ikijumuisha
nyumba nyingi kupasuka (Picha Namba 3 na 4), watu wengi kujeruhiwa kwa
kuangukiwa na vifusi na kuta za nyuma ambapo inakisiwa kuwa watu 13
wamepoteza maisha yao.
Picha namba 4: Nyumba ziliyobomolewa na tetemeko la ardhi Bukoba.
2 Sababu za kutokea tetemeko hilo:
Kwa kuwa kitovu cha tetemeko hilo kiko chini sana ya ardhi (Km 10) na
kwa kutafasiri umbile la mawimbi ya tetemeko hilo yaliyonakiliwa na
vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi (Picka Namba 5) inaonekana kuwa
tetemeko hilo limetokana na misuguano ya mapange makubwa ya ardhi
iliyopasuliwa na mipasuko ya ardhi mithili ya mipasuko kwenye bonde la
ufa. Kwa kuwa eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi liko karibu na
mkondo wa magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki inakisiwa kuwa
mtetemo huu umesababishwa na kuteleza na kusiguana ka mapande ya miamba
juu ya mipasuko ya ardhi ya bonde hilo la ufa.
Picha Namba 5: Umbile la mawimbi ya tetemeko la ardhi la tarehe 10 Septemba mkoani Kagera.
3 Upimaji wa matetemeko ya ardhi.
Mapaka sasa na duniani kote hakuna vifaa au taratibu za kuweza
kutabiri utokeaji wa matetemeko ya ardhi. Vifaa vyote na taratibu zote
za kuratibu/kupima matetemeko ya ardhi vinapima ukubwa na tabia ya
tetemeko baada ya tetemeko kutokea.
4 Tafiti za kina.
Wakala wa Jiolojia Tanzania umepeleka wataalamu katika eneo la tukio
ili kuendelea kufanya utafiti wa kina juu ya tetemeko hilo. Taarifa
zaidi juu ya tukio hili zitaendelea kutolewa kulingana na matokeo ya
tafiti hizo pamoja na tafasiri ya taarifa na takwimu za matetemeko ya
ardhi zinazonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi nchini
hususan kituo cha Geita ambacho ndicho kilicho karibu sana na eneo la
tetemeko hili .
5 Mambo Muhimu ya Kuzingatia Kuepuka Madhara Yanayoweza Kusababishwa na Tetemeko la Ardhi
i. Kabla ya tukio:
(a) Elimu ya tahadhari inapaswa itolewe ili kila mmoja aelewe nini
cha kufanya linapotokea tetemeko la ardhi ikiwa ni pamoja na kupata
mafunzo kutoka kwa watu wa msalaba mwekundu kuhusu namna ya kuhudumia
majeruhi ama wahanga na pia jeshi la zima moto ili kupata elimu kuhusu
namna ya kutumia kizimamoto. Elimu na mafunzo hayo yatasaidia kuwaweka
watu katika hali ya tahadhari na hii itasaidia kupunguza taharuki wakati
wa tukio kwa vile watakuwa sasa wanajua namna ya kuchukua tahadhari.
(b) Kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari hizo mara kwa mara ili
kujizoesha kwani mara nyingi wakati wa matukio ya majanga kama hayo watu
huchelewa kuchukua uamuzi wa haraka kujinusuru kwani huwa bado
wanajiuliza kwamba wafanye nini. Hivyo mazoezi ya mara kwa mara ya jinsi
ya kuchukua tahadhari humfanya mtu kufanya uamuzi wa haraka pindi tukio
linapotokea.
(c) Wananchi pia wanashauriwa kujenga nyumba bora na imara kwa
kuzingatia viwango halisi vya ujenzi, kuweka misingi imara wakati wa
ujenzi, kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa
kujengwa katika eneo husika kulingana na ardhi ya mahali hapo, kuepuka
ujenzi wa nyumba katika miinuko mikali yenye kuambatana na mawe/ miamba
(suspended boulders) na kuepuka ujenzi wa makazi katika maeneo tete
yenye mipasuko ya miamba (faults) na uwezekano mkubwa wa kutokea
matetemeko.
ii Wakati wa tukio:
(a) Wakati wa tukio la tetemeko la ardhi unashauriwa kukaa mahali
salama kama vile sehemu ya wazi isiyo na majengo marefu, miti mirefu na
miinuko mikali ya ardhi. Watu wanashauriwa kukaa nje ya nyumba katika
sehemu za uwazi.
(b) Endapo tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba unashauriwa ukae
chini ya uvungu wa meza imara, ama kusimama kwenye makutano ya kuta na
pia ukae mbali na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au fenicha ili
kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo.
(c) Unashauriwa usitembee umbali mrefu kwa lengo la kutafuta mahali
salama kwa sababu tetemeko la ardhi hutokea ghafla na huchukua muda
mfupi. Takwimu zinaonesha kwamba watu wanaotaharuki na kukimbia ovyo
wakati wa tukio la tetemeko ndio hupata madhara ama kuumia.
(d) Salimisha macho yako kwa kuinamisha kichwa chako wakati wa tukio.
(e) Baki mahali salama hadi hapo mitetemo itakapo malizika na kisha
ujikague kuona kama hujaumia na ndipo utoe msaada kwa wengine ambao
watakuwa wameumia.
(f) Ondoka mahali ulipo kwa uangalifu kuepuka vitu ambavyo vitakuwa vimedondoka na kuvunjika kwani vinaweza kukudhuru.
(g) Jiandae kwa mitetemo itakayofuata baada ya mtetemo mkuu. Tetemeko
kuu huwa mara nyingi linafuatiwa na mitetemo mingi midogo midogo.
(h) Kumbuka kuwa matukio ya matetemeko ya ardhi huweza kuambatana na
moto hivyo jihadhari na matukio ya moto kwa vile tetemeko la ardhi
linaweza kusababisha kupasuka kwa mabomba ya gesi au kukatika kwa nyaya
za umeme ama kuharibika kwa vifaa vinavyotumia umeme na kusababisha
hitilafu ya umeme.
(i) Kama uko nje ya jengo wakati tetemeko linatokea unashauriwa
kubaki nje, simama mahali pa wazi na uwe mbali na majengo, miti mikubwa,
nguzo na nyaya za umeme na ujikinge kichwani kadri inavyowezekana kwani
paa za nyumba, miti, nguzo na nyaya za umeme vinaweza kudondoka na
kuleta madhara.
(j) Endapo utakuwa unaendesha chombo cha moto wakati wa tukio la
tetemeko la ardhi unashauriwa usimame kwa uangalifu sehemu salama na
usubiri hadi mitetemo imalizike ndipo uendelee na safari yako kwani
tetemeko linaweza kusababisha barabara au madaraja kukatika.
(k) Endapo utakuwa kwenye maeneo ya miinuko au milima uwe mwangalifu ili kuepuka kuporomokewa na mawe au kuangukiwa na miti,
(l) Baada ya mitetemo kumalizika endapo itakulazimu kuondoka mahali
ulipo ukiwa katika jengo refu unashauriwa kutumia ngazi badala ya lifti
au kipandishi.
iii Baada ya tukio:
(a) Wananchi wanashauriwa baada ya tukio kuzima umeme katika majengo
ili kuepuka kutokea kwa hitilafu ya umeme kwani mitetemo huenda
ikaendelea tena.
(b) Kukagua majengo kwa uangalifu ili kuhakikisha kama hayakupata
madhara kama vile nyufa n.k,na kwamba yanaweza kuendelea kutumika na
kama ikibidi basi unashauriwa kuwaita wataalamu wa majengo ili
wayafanyie ukaguzi.
(c) Endapo utaangukiwa na vitu vizito usijaribu kutumia nguvu nyingi
ili kujinasua kwani hujui vitu hivyo vina uzito kiasi gani, omba msaada
kwa kuita kwa sauti lakini usifanye hivyo mara nyingi ili usipoteze
nguvu nyingi mwilini maana hujui ni lini utaokolewa,
(d) Toa msaada unaowezekana kwa watu walioathirika na tetemeko na utoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika na uokoaji.
No comments