Header Ads

Uingereza Yachangia Bilioni 6 kwa Ajili ya Ukarabati wa Shule Mkoani Kagera

Uingereza imetoa mchango wa Shilingi Bilioni 6 kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule zilizopata madhara kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea katika Mkoa wa Kagera tarehe 10 Septemba, 2016.

Mchango wa fedha hizo umewasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Catherine Cooke, Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Balozi huyo kuwasilisha hati zake za utambulisho.

Balozi Sarah Catherine Cooke amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na kutoa mchango wa fedha hizo Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May anatoa pole kwa Serikali ya Tanzania na kwa familia zote zilizopatwa na madhara ya tetemeko hilo na kwamba Uingereza imeona ishirikiane na Tanzania katika kukabiliana na madhara hayo.
“Uingereza imeguswa sana na maafa yaliyowakumba wananchi kufuatia tetemeko lililotokea Kagera, tunapenda kuona wananchi wanasaidiwa na wanafunzi wanaendelea na masomo” amesema Balozi Sarah Catherine Cooke.

Kwa Upande wake Rais Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu wa Uingereza kwa mchango huo ambao utasaidia juhudi za Serikali za kuhakikisha inarejesha miundombinu iliyoharibika zikiwemo shule.

“Mhe. Balozi Sarah Catherine Cooke naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May na umueleze kuwa kwa niaba ya watanzania hususani waliopatwa na madhara ya tetemeko la ardhi tumeguswa sana na moyo wake wa upendo kwetu” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli na Balozi Sarah Catherine Cooke pia wamezungumzia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uingereza ambapo Rais Magufuli ametoa wito kwa Balozi huyo kuendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Uingereza kuongeza uwekezaji wao hapa nchini na kwamba Tanzania itaendeleza na kukuza uhusiano huo.

“Uingereza ni rafiki na ndugu wa kweli na wa kihistoria kwa Tanzania, tunatambua kuwa nchi yenu ni mdau mkubwa na muhimu wa maendeleo yetu, hivyo tusingependa kupoteza rafiki na ndugu yetu, tuendelee kushirikiana kwa manufaa ya wananchi.

“Natambua kuwa Uingereza ina utaalamu mkubwa katika masuala ya gesi hivyo nawakaribisha waje wawekeze katika sekta ya gesi” amesisitiza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amesema Serikali itahakikisha fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na madhara ya maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera zinafikishwa kwa walengwa na ameonya kuwa watakaothubutu kuiba fedha hizo watashughulikiwa.

Dkt. Magufuli amebainisha kuwa baada ya kutengua uteuzi na kuchukua hatua nyingine dhidi ya aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Amantius Msole na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Bw. Steven Makonda pamoja na kumsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bw. Simbaufoo Swai, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei awachukulie hatua watumishi wa Benki hiyo walioshirikiana na watumishi hao kufanya njama za kuanzisha akaunti nyingine ya benki yenye jina linalofanana na akaunti rasmi ya “Kamati ya Maafa Kagera” kwa lengo la kujipatia fedha”

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

28 Septemba, 2016

No comments

Powered by Blogger.