Header Ads

Aukumiwa jela miaka 15 kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria

Mkazi mmoja wa jijini hapa, Said Shomari (64) amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Shomari ambaye ni fundi saa, alitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo baada ya mshtakiwa kukiri kosa hilo.

Alikiri kutenda kosa hilo jana alipopandishwa kizimbani mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Adolf Mkini kumsomea mashtaka yaliyokuwa yakimkabili kwa lengo la kumkumbusha, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.

Katika kesi hiyo, Shomari alishtakiwa na mtoto wake, mfanyabiashara Ramadhani Said (40), kwa makosa mawili, moja la kukutwa na silaha na la pili la kukutwa na risasi bila kibali na kinyume cha sheria.

Katika mashtaka hayo, Shomari alikiri kosa moja la kumiliki silaha na akakana kosa la kumiliki risasi kinyume cha sheria.

Hata hivyo, wakati Shomari akikiri kutenda kosa hilo moja na kuhukumiwa adhabu hiyo, mtoto wake alikana kutenda makosa hayo yote.

Awali, akiwasomea mashtaka hayo, Wakili Mkini alidai kuwa Novemba 9, 2015, eneo la Kigogo, wilayani Ilala, mshtakiwa alikutwa akimiliki bastola moja ndogo pamoja na risasi moja bila kuwa na kibali.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo na kuulizwa kama ni kweli au si kweli, ndipo alipokiri kutenda kosa hilo kwa kujibu kuwa ni kweli, hivyo Mahakama ikamtia hatiani.

“Kwa kuwa mshtakiwa amekiri kutenda kosa kwa shtaka linalomkabili, Mahakama inamtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela.”, alisema hakimu Mashauri.

Baada ya kutoa hukumu hiyo aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 15, mwaka huu, wakati kesi hiyo itakapoendelea kusikilizwa shtaka moja kwa upande wa Shomari na mashtaka yote mawili kwa upande wa Ramadhani.

No comments

Powered by Blogger.