Header Ads

Lowassa na Sumaye wapewa MAKAVU ndani ya mkutano mkuu wa CCM .........

Vigogo mashuhuri wa Chadema waliowahi kuwa mawaziri wakuu; Edward Lowassa na Frederick Sumaye, jana waligeuka gumzo ndani ya Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kumchagua Rais John Magufuli, kuwa Mwenyekiti wa tano wa chama hicho.

Gumzo hilo, lilianzishwa na Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba, alimpomtaka Askofu wa Kanisa la Ufufuko na Uzima, Josephat Gwajima, asimpotoshe Magufuli ili yasije yakampata ya Sumaye, ambaye sasa anachezea mchangani Kibaha.

Sumaye mchangani
“Hata akina Sumaye hawakuunda vyama vyao. Bado wanahangaika; na sasa Sumaye anacheza mchangani Kibaha,” alisema Makamba.

Sumaye ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu na NEC ya CCM, kwa sasa anawania uongozi wa Kanda ya Pwani katika Chadema. Kabla ya kusema kuwa Sumaye anahangaika na siasa za mchangani, Makamba alimtaka Gwajima kuacha uongo na kusingizia viongozi wa CCM.

Makamba aliyepewa nafasi ya kumuombea kura Rais John Magufuli kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, alisema anamtia moyo Magufuli asiogope kuongoza chama, kwani hataongoza peke yake bali wapo wanachama wengi watakaomsaidia kazi hiyo.

“Wewe siyo wa kwanza kukataa kazi hii. Hata watangulizi wako Kikwete na Benjamin Mkapa nao walifanya hivyo hivyo,“ alisema Makamba ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Makamba alisema hata manabii na mitume wengi, kama Haruni, Mussa, Yona au Yunus na Yeremia walifanya vivyo hivyo, walipopewa utume au unabii na Mungu, kwani waliogopa kufanya kazi hizo lakini, alisema mara zote Mungu aliwaagiza kuwa wasiogope kuwa manabii na mitume, kwani atatia maneno kwenye vinywa vyao.

Aidha, Makamba alitaka viongozi wa dini mfano Askofu Gwajima, waache kumfitini Kikwete eti kwamba alikuwa hataki kumpa uenyekiti Magufuli.

“Askofu Gwajima alikuwa anasingizia kuwa Jakaya kiongozi wetu mpendwa hataki kukupa uenyekiti. Alikuwa akikuhimiza kuwa kama hataki uunde chama chako. Huu ni uongo. Gwajima amemaliza uongo wote,” alisema Makamba na kumuomba Magufuli asisikilize uongo wa kiongozi huyo wa kiroho.

Makamba alimtaka Askofu Gwajima atambue kuwa hata baadhi ya wana-CCM waliojiengua mwaka jana, hawakuunda vyama vyao badala yake wameangukia pua.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo, kumpa kura zote za ‘Ndiyo’ Rais Magufuli, kisha Makamba akaanza kutumia uhodari wake wa misemo, methali, mafumbo na aya za Biblia na Kurani Tukufu.

“Mzigo wa chama ulikuwa umebebwa na Mkwere Kikwete ambaye sasa anaondoka; na kwa kuwa kuna msemo kuwa ‘mzigo mzito mpe Mnyamwezi au Msukuma, nawaomba wajumbe wote sasa mzigo wa chama tumpe Msukuma Magufuli,” alisema na kauli yake hiyo ilishangiliwa na wajumbe.

Lowassa na ufisadi
Akielezea aina ya kiongozi anayetoka CCM na anayeingia, Makamba alisema kuwa anayetoka, Kikwete ni mpiganaji wa ufisadi, kwa kuwa alifikia hatua ya kumtosa rafiki yake Edward Lowassa, kuwa hafai kuwa Rais kwa kuwa anatuhumiwa kwa ufisadi.

Alisema kada wa chama hicho anayeingia baada ya Kikwete, Dk Magufuli yeye ndiye muasisi wa Mahakama ya Mafisadi, ambayo tayari imeshaanzishwa kwa Sheria ya Bunge. Kwa mujibu wa Makamba, Kikwete ni kiongozi aliyepiga vita umasikini na anapoondoka, anayeingia Dk Magufuli msimamo wake ni asiyefanya kazi na asile.

Kumchinja Kobe
Naye mmoja wa vigogo wa Chadema aliyerejea CCM, Fred Mpendazoe, alikuja na dhana ya namna ya kumchinja kobe, akifananisha na utaratibu uliotumika, kukata jina la Lowassa katika majina 38 ya wagombea urais.

Mpendazoe alisema Kikwete alifanya ‘timing’ sana kushughulikia ufisadi ndani ya chama hicho, kwa kuwa kati ya makada hao 38 waliokuwa wakiwania urais, baadhi akiwemo Lowassa walikuwa na tuhuma za ufisadi na kukatwa kwa majina yao, kulifanyika kwa wakati sahihi.

Kuachana na nzi
Mpendazoe pia alisema Wasambaa walimfundisha msemo mmoja kwamba, mtu akitaka asifuatwe na nzi, anatakiwa atupe mzoga na kuongeza kuwa, hatua ya wagombea wenye tuhuma za rushwa kutupwa, CCM ilitupa kibudu.

Kwa mujibu wa Mpendazoe, kuhamia Chadema kwa Lowassa, kulisababisha chama hicho na Ukawa waliomuunga mkono, kupoteza ajenda, kwa kuwa walimpokea mtu waliyezunguka nchi nzima wakimtuhumu kwa ufisadi tena wakisema wanao ushahidi.

“Walipompokea Lowassa, nikasema basi mchezo umekwisha wamepoteza ajenda,” alisema Mpendazoe huku akishangaa kitendo cha Ukawa kudai demokrasia imekuwa ikibanwa.

Gia angani
Mpendazoe alisema anashangaa kusikia Magufuli anabana demokrasia na kuhoji kati ya chama kilichotangaza nafasi ya urais na kuruhusu wagombea 38 kugombea, huku mchujo ukifanyika hadharani na kilichompata mgombea kwenye chopa (helikopta), ni kipi chenye demokrasia?

Akifafanua zaidi, Mpendazoe alisema Chadema ilimpata mgombea wake angani ndani ya helikopta, na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe alipokwenda katika vikao, akasema chama hicho kimebadilisha gia angani.

“Nilihoji iweje uamuzi huo ufanyike bila vikao,” alisema na kuongeza kuwa kilichofanyika kilikuwa sawa na biashara na kuhoji kwa nini chama hicho kisisajiliwe Brela (Ofisi ya Msajili wa Makampuni) ili kufanya biashara.

CCM B
Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alihoji yeye kuitwa CCM B, baada ya Rais Magufuli kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole na kusema inakuwaje yeye aliyetoka katika chama hicho mwaka 1995, apewe jina hilo.

Alisema kama kupewa cheo na Magufuli, ndio sababu ya kuitwa CCM B, basi hata Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, ni CCM B kwa kuwa aliteuliwa kuwa Mbunge na Rais Jakaya Kikwete.

Mrema alisema kama kuitwa kwake CCM B ni kutokana na kutoka ndani ya CCM; basi Lowassa na Sumaye ni CCM A, kwa kuwa wao wametoka mwaka jana wakati yeye ametoka tangu 1995.

Haeleweki
Naye Magufuli alisema alimshangaa Rais mstaafu Benjamini Mkapa, kwa kumteua mtu mmoja kuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo, wakati waliofanyakazi na Waziri Mkuu huyo, akiwamo yeye waliona kuwa ni mtu asiyeeleweka. Waziri Mkuu wa Mkapa, alikuwa Frederick Sumaye.

Kauli hiyo ya Magufuli, ilitanguliwa na ya Kikwete, ambaye alishangaa kuona mtu aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, sasa anagombea uenyekiti wa Kanda.

No comments

Powered by Blogger.