Header Ads

Bunge latenga fungu kwa ajili ya safari za Ulaya na Marekani

Wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikizuia maofisa na watumishi wa umma kwenda nje ya nchi kwa safari ambazo si za lazima ili kubana matumizi, Bunge limesema limetenga fungu kwa ajili ya kuwawezesha wabunge kupata mafunzo ya uendeshaji bora wa Bunge nje ya nchi.

Novemba 7, mwaka jana, ikiwa ni siku mbili tu baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tano, John Magufuli alipiga marufuku safari za nje kwa maofisa wa serikali isipokuwa tu itakapokuwa lazima na kwa ruhusa ya Ikulu.

Rais Magufuli alisema shughuli nyingi za nje ya nchi zitafanywa na kusimamiwa na mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi hizo.

Wakati Rais Magufuli akitekeleza sera yake ya 'Hapa Kazi Tu' kwa kubana matumizi kiasi cha kuzuia semina elekezi kwa mawaziri ambayo ingeharimu Sh. bilioni mbili, uongozi wa Bunge jana ulisema umepanga kupeleka wabunge ughaibuni kwa ajili ya mafunzo.

Akifungua semina ya wenyeviti wa kamati za Bunge iliyofanyika mjini hapa jana, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema uongozi wa Bunge hilo utaandaa mafunzo kwa vitendo nje ya nchi kwa ajili ya wabunge.

"Katika siku za usoni, pia tutaandaa mafunzo haya kwa vitendo nje ya nchi. Lipo Bunge moja tu Tanzania; na hivyo mafunzo pekee ya vitendo ni kwa kutembelea mabunge ya wenzetu," alisema Ndugai na kuibuka shangwe za wenyeviti wa kamati za Bunge ukumbini.

Baadhi yao walimuomba arudie kuelezea dhamira hiyo. "Nafurahi kwamba tuna mawasiliano mazuri na mabunge mengi ya nchi zinazoendelea kama vile Uingereza, India na hata Marekani," alisema Ndugai ambaye Bunge lake, kwa vyovyote, limeathiriwa na mkakati wa serikali wa kubana matumizi.

"Lakini pia kwa majirani zetu hapa, yaani Zambia, Kenya, Uganda, Afrika Kusini na kadhalika. Tutatumia ujirani na uhusiano wetu na mabunge hayo ili mfaidike kwa mafunzo."

Baada ya kufungua rasmi mafunzo hayo, Ndugai alisema kuwa wameona kuna ulazima wa kuwa na mafunzo kwa wabunge ndani na nje ya nchi kutokana na wengi wao kuwa wageni wa uendeshaji wa Bunge.

"Kazi ni kubwa sana (kuedesha shughuli za Bunge). Ni kama tunaanza upya kwa sababu wabunge wengi ni wapya," alisema.

"Tumeamua kuwa na mafunzo haya ili kuwa na uelewa wa pamoja na kuwa na uendeshaji bora wa bunge."

Ndugai alisema kutakuwa na mafunzo ndani na nje ya nchi kwa makundi mbalimbali yakiwamo ya wabunge wote, wanawake, vijana, viongozi wa wabunge na kamati za Bunge.

Aliongeza kuwa tayari kuna fungu ambalo limetengwa kwa ajili ya kugharamia mafunzo hayo, lakini hakuwa tayari kuanika kiasi cha fedha kilichotengwa, hata hivyo.Alipoulizwa kuhusu kukinzana na agizo la Rais Magufuli, Spika huyo alisema:

"Ni kweli kwamba alichosema Mheshimiwa Rais cha kupunguza safari za nje. Sisi (Bunge) pia tumejitahidi sana kupunguza safari za nje, lakini katika mafunzo haya, inafikia wakati mtu lazima aone Bunge jingine linafanya nini.

"Wajue nao wenzao duniani wanafanya nini. Ila wasiwe wengi na haitakuwa mara kwa mara." Ndugai pia alilimwagia sifa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kufadhili mafunzo ya wabunge, ikiwamo semina ya jana, kupitia mradi wa wake wa kusaidia mabunge (LSP).

Alisema mradi huo umekuwa ukisaidia kutoa semina kwa kamati mbalimbali za Bunge ili kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati hizo katika kutekeleza majukumu yao ya kikatiba kwa ufanisi zaidi.

Alisema mradi huo ulioanza rasmi 2011, utamalizika mwezi ujao, lakini mazungumzo yanaendelea ili uendelee hadi 2020 na kwamba wafadhili wameonyesha nia ya kuendelea katika Bunge la 11 kuanzia Julai, mwaka huu hadi Juni, 2020.

Katika semina ya jana ambayo Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alishiriki, kulikuwa na mafunzo ya mchakato wa kutunga sheria na uchambuzi wa miswada, mchakato wa maandalizi ya Bajeti ya Serikali na Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 pamoja na majukumu wenyeviti wa kamati za Bunge na namna ya kuzungumza mbele ya hadhara.

Semina hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Naibu Kamishna wa Bajeti - Mikoa na Halmashauri, Dk. Charles Mwamwaja na mawakili Said Yakubu na Harold Sungusia waliokuwa watoa mada, kulikuwa na mafunzo ya namna ya kutumia vyombo vya habari wakati wa shughuli za kamati na mabadiliko, maboresho na hatma ya Bunge.

Masharti
Mwishoni mwa mwaka jana, Ofisi ya Rais ilisambaza mwongozo kwa taasisi na mashirika ya umma unaoweka masharti ambayo watumishi wa umma wanaotaka kusafiri nje ya nchi watatakiwa kuyatimiza ili wapewe kibali cha kusafiri.

Masharti hayo ni kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi na maombi hayo yawasilishwe kwa Msajili wa Hazina kabla ya kwenda Ikulu ili mwombaji aweze kujenga hoja kwa kuzingatia umuhimu wa safari hiyo na tija itakayopatikana kutokana na safari hiyo.

Masharti hayo yanamtaka Mtendaji Mkuu wa Shirika ama taasisi kama Bunge, apime kama safari hiyo ni muhimu kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi kabla ya kuwasilishwa Hazina.

Sharti lingine ni kupima umuhimu wa safari hiyo na kuona isipofanyika itaathiri vipi taifa, na mwombaji aeleze manufaa ya safari hiyo kwa taasisi na taifa kama imewahi kufanyika huko nyuma.

Ofisi za Umma zilipokea barua kutoka kwa Msajili wa Hazina Novemba 12, mwaka jana zikieleza kuwa Rais Magufuli ametoa zuio la jumla kwa safari za nje ya nchi katika utumishi wote wa umma na mihimili yake.

Barua hiyo ya Hazina ilisema zuio hilo litadumu hadi pale itakavyoelekezwa vinginevyo.

 Akihutubia katika ufunguzi wa Bunge la 11 Novemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli alisema safari za nje katika mwaka mmoja na nusu wa mwisho ya awamu ya nne zilitafuna zaidi ya Sh. bilioni 4, kiasi ambacho kingeweza kujenga kilometa 40 za barabara ya lami

No comments

Powered by Blogger.