RIPOTI YA CAG: Vyama vya siasa vyakacha ukaguzi
Dodoma. Kati ya vyama 22 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, ni chama kimoja tukilichopeleka hesabu zake kukaguliwa kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzoni mwaka 2015.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, alikitaja chama hicho kuwa ni Chama cha Wananchi (CUF), kilichopeleka hesabu zake za kuanzia Januari mpaka Juni 2015, huku vyama vingine 21 vikishindwa kufanya hivyo, kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 14 cha sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992.
“...na hili lifahamike kuwa, siyo katika kipindi hicho, hata leo (jana) nimeuliza wasaidizi wangu kama wameshaleta au bado lakini naambiwa ni chama kimoja,” alisema.
Alipendekeza ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kufuatilia suala hilo ili uwasilishaji wa taarifa za fedha ufanywe kwa wakati kulingana na matakwa ya kisheria.
Nyama hatari
Katika hatua nyingine, Profesa Assad alibainisha kuwa, Watanzania wengi wanakula nyama zisizo salama na hivyo afya zao kuwa shakani.
Alisema hakuna uhakika wa nyama inayotumiwa na Watanzania kama ni salama kwa matumizi ya binadamu, huku akizishukia mamlaka zinazotoa kibali kwa kuruhusu mwanya wa kusajili machinjio yasiyokidhi vigezo.
Alisema katika ukaguzi wa ofisi yake, walibaini katika machinjio mbalimbali, asilimia 75 yalikuwa yanafanya kazi katika hali ya uchafu ikiwamo wahusika kushindwa kunawa miguu na mikono wanapotoka kujisaidia.
Kwa mujibu wa Profesa Assad, upungufu alioubaini unatokana na kuwapo kwa taasisi zaidi ya moja zilizopewa jukumu la kusajili machinjio, hatua aliyosema inasababisha mkanganyiko.
Alisema machinjio sita kati ya 12 (sawa na asilimia 50) kwenye halmashauri saba walizotembelea, hazikuwa zimesajiliwa na mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kutokana na kutokidhi vigezo.
Aidha, machinjio 10 kati ya 12 (asilimia 83) hayakusajiliwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi kutokana na kutokidhi viwango, lakini yalikuwa yanaendelea kufanya kazi.
CAG alipendekeza wizara husika kuanzisha mfumo madhubuti wa kukagua nyama katika machinjio yote nchini.
No comments