Header Ads

Mahakama ya mafisadi kuanza Julai mwakaa huu.......

WAKATI Rais John Magufuli akisisitiza kuwa utumbuaji majipu utaendelea kufanyika hadharani bila kificho, pigo jingine kwa waliotumbuliwa na wanaosubiri kutumbuliwa, limetangazwa.

Akisoma Mwelekeo wa Kazi za Serikali bungeni jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mbali na kusisitiza kuendelea kushughulikia watendaji wazembe, wabadhirifu na wavivu, alitangaza kuwa Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi imeanzishwa katika Mahakama Kuu na itaanza kazi zake Julai mwaka huu.

Hatua hiyo ni pigo kwa watuhumiwa wa ufisadi ambao tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, wamekuwa wakichukuliwa hatua hadharani ya kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zao, kiasi cha baadhi ya wanasiasa kushindwa kuvumilia na kujitokeza kulalamika.

Miongoni mwa wanasiasa waliojitokeza kulalamikia hatua ya watuhumiwa hao kuchukuliwa hatua ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Edward Lowassa.

Mahakama ya Rushwa
Mahakama hiyo ni moja ya ahadi zilizonadiwa na Dk Magufuli katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, akisema katika Hotuba ya Ufunguzi wa Bunge na kuirejea wakati wa uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama na Siku ya Sheria Duniani.

Katika maandalizi ya uundwaji wake, Jaji Kiongozi, Shaban Lila, aliwahi kusema kwamba mahakama iliitisha wadau mbalimbali wa haki jinai, kuangalia namna ya kuanzisha mahakama hiyo, ambapo mjadala ulikuwa ni kuanzisha mahakama huru au kitengo maalumu ndani ya Mahakama Kuu, kitakachopewa kipaumbele cha kushughulikia mafisadi.

Akitangaza kukamilika kwa mchakato huo jana, Waziri Mkuu Majaliwa alisema: “Napenda kuliarifu Bunge kwamba Serikali imeanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza kufanya kazi Julai, 2016.”

Uharaka wa kesi
Mbali na kuanza kufanya kazi kwa mahakama hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa pia alisema kuwa Serikali itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ili ziharakishe utoaji wa haki.

Uimarishwaji wa ofisi hizo pia unatokana na agizo la Rais Magufuli alilotoa siku hiyo ya uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama na Siku ya Sheria Duniani, alipotaka kesi za uhujumu uchumi na ufisadi ziendeshwe kwa kasi, ili jitihada za Serikali za kupambana na matatizo hayo, zizae matunda.

Katika hotuba hiyo ya Siku ya Sheria Duniani, Rais Magufuli alielezea kushangazwa na kitendo cha ofisi ya DPP, kuchelewa kuwapeleka mahakamani watuhumiwa waliokamatwa na ushahidi.

Alitoa mfano wa watuhumiwa waliokamatwa na meno ya tembo, ambapo alitaja Mahakama ya Kisutu kuwa ilikuwa na kesi 26 za watu walioshikwa wakiwa na nyara za Serikali, lakini kesi hizo zikachukua zaidi ya miaka mitano bila kufanyiwa uamuzi.

Dk Magufuli alisema maelezo yaliyokuwa yakitolewa ni kwamba upelelezi bado unaendelea wakati wahusika wa kufanya upelelezi huo wapo na washitakiwa walishikwa wakiwa na vielelezo.

Alisema inawezekana hakimu akawa anataka kutoa hukumu, lakini DPP na Polisi wanaofanya uchunguzi, wanasema upelelezi unaendelea, jambo linaloonesha tatizo lililopo la ucheleweshaji kesi.

Utumbuaji kuendelea
Katika hotuba hiyo ya Majaliwa, iliyokwenda sambamba na makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2016/17, alisema Serikali itaendelea kuwawajibisha wale wote ambao hawataendana na Falsafa na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano, lakini akasisitiza kwamba serikali itachukua hatua kwa kuzingatia na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.

“Niwahakikishie Watanzania kwamba hakuna mtumishi au mwananchi atakayeonewa au kunyanyaswa katika hili. Hivyo wale wote ambao wako safi waendelee kutimiza wajibu wao bila woga. Kazi zifanyike kwa weledi na kwa kasi bila urasimu,” alisema.

Majaliwa alisema katika kutekeleza falsafa ya Hapa Kazi Tu na ili Tanzania ifikie uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 ni sharti kila mtu afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu wa hali ya juu.

“Ili yawepo mapinduzi ya kweli ya kuelekea kwenye uchumi wa Kati tunaodhamiria ni lazima tuimarishe uwajibikaji na maadili kwa viongozi, watendaji na kwa kila Mtanzania. Sote tumeshuhudia hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya watumishi wasio waadilifu, wanaotumia fedha za umma na madaraka yao vibaya.

“Ndio maana tumeanza kwa nguvu kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma ili zielekezwe kwenye shughuli zenye manufaa kwa Watanzania walio wengi na si vinginevyo,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumzia utekelezaji wa Sera ya Utoaji Elimu Bure kuanzia Darasa la Kwanza hadi Kidato cha Nne, Waziri Mkuu Majaliwa alisema ipo changamoto ya upungufu mkubwa wa madawati baada ya kuanza kuandikisha watoto shule bila malipo.

Kutokana na hilo, aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini waliokamata mbao kutokana na makosa mbalimbali kutozipiga mnada mbao hizo na badala yake watumie mbao hizo kutengeneza madawati kuanzia jana na pia halmashauri kutumia rasilimali zake kutengeneza madawati kwa kila shule.

No comments

Powered by Blogger.