Header Ads

Lowassa, UKAWA motomoto mafuriko yatanda kila kona...Huku wanachama wakongwe wakihama CCM

Kambi kuu ya upinzani katika siasa za Tanzania, imezidi kuimarika. Matukio mawili, moja la jana, jingine leo hii, yametokea na kuongeza nguvu ya kampeni ya kuitoa CCM madarakani chini ya kaulimbiu ya “Toroka uje.”

Katika tukio la kwanza jana jioni, kambi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ilimpokea Omari Ayubu Kimbau, kada machachari wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akihamia Chama cha Wananchi (CUF) anakotarajia kupewa dhamana ya kugombea ubunge jimboni Mafia, Mkoa wa Pwani.

Kimbau ni mmoja wa watoto wa Kanali Ayubu Shomari Mohamed Kimbau, mwanasiasa mstaafu aliyekuwa mbunge wa muda mrefu wilayani Mafia.
Uamuzi wa Kimbau kuhama CCM umefanikishwa mara tu alipobaini kudhulumiwa kisiasa kulikotimia juzi kwa kutupwa nje ya mbio za uteuzi ka mara ya pili mfululizo, ili kugombea ubunge.

Tayari mipango ya kumkabidhisha bendera ya kugombea kiti hicho kupitia CUF, inakamilishwa na taarifa za ndani ya CUF zinasema atatambulishwa rasmi jimboni Jumatano wiki ijayo.

Kimbau amekosa uteuzi katika vikao vya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC-CCM) vilivyomalizika mwishoni mwa wiki mjini Dodoma, ambako ugombeaji alipewa Mbaraka Dau, ndugu wa damu wa Dk. Ramadhan Dau, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Katika kura za maoni zilizohusisha matawi ya CCM jimboni, Kimbau alipata kura 1,480 huku Dau anayeishi Dubai, kwa shughuli za biashara, akipata kura 2,620. Injinia Omari Kipanga alipata kura 1,156; Shah 568 na Njalale 23.

Jimbo la Mafia ambalo Abdulkarim Shah (Bulji) ameliwakilisha vipindi viwili, kwa makubaliano ya UKAWA, limeachwa ligombewe na mwakilishi atokaye CUF, chama chenye historia ya kuwa ngome kwa CCM wilayani Mafia.

Wachambuzi wa siasa za Mafia, wanasema Kimbau ameingia kambi ya UKAWA akiwa na mtaji wa zaidi ya wanachama 6,900 waliohakikiwa kujiunga Chadema kufikia sasa; CUF zaidi ya 6,000; watu 1,480 waliompigia kura za maoni CCM.

Tukio la pili ni la jijini Arusha ambako mgombea urais anayewakilisha UKAWA, Edward Lowassa, amefanya mkutano mkubwa wa hadhara wa kutambulishwa na kupata wadhamini, ametinga kambini Lawrance Masha.

Masha, waziri wa mambo ya ndani kwa awamu ya kwanza ya serikali ya Rais Jakaya Kikwete (Novemba 2005/2010), alipigwa kumbo katika uchaguzi mkuu uliopita, jimbo la Nyamagana, jijini Mwanza analowakilisha Ezekiel Wenje.

“Maamuzi magumu yamefanyika hivi leo, lakini ni maamuzi muhimu sitaongea leo. Nitangaze tu kwamba nimejiunga rasmi Chadema,” amewaambia wana-UKAWA waliojazana viwanja vya Tindigani.

 Masha ni mtoto wa Dk. Fortunatus Masha, aliyestaafu siasa akiwa Chama cha United Democratic Party (UDP) alikofikia ngazi ya makamu mwenyekiti.

Amehama CCM siku chache baada ya kuthibitisha kutupwa na CCM katika uteuzi kutokana na kushindwa kura za maoni safari hii akiwinda jimbo la Sengerema.

Baada ya mkutano wa Arusha, Lowassa, ambaye alihama CCM tarehe 28 Julai akijibu pigo la kukatwa jina katika walioomba uteuzi wa kugombea urais, akiwa miongoni mwa waombaji 38, atakuwa jijini Mwanza kesho Jumapili.

No comments

Powered by Blogger.